MWILI WA MWANASIASA MKONGWE NDEJEMBI KUZIKWA KESHO DODOMA

Mwili wa mwanasiasa mkongwe nchini Pancras Ndejembi unatarajia kuzikwa kesho Jumanne Januari Mosi, 2019 katika kitongoji cha Chizomoche kijiji cha Bihawana Jijini Dodoma.

Ndejembi (90) alifariki dunia Jumamosi Desemba 29, 2018 saa 2 asubuhi katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Dodoma.

Mweyekiti wa kamati ya mazishi, David Mzuri amesema leo Jumatatu Desemba 31, 2018 kuwa maandalizi yote yamekamilika ikiwemo watoto wa marehemu ambao walikuwa wanasubiriwa kutoka nje ya nchi.

Mzuri amesema mwili wa marehemu ulitarajia kuchukuliwa hospitali leo na kulala nyumbani kwake mtaa wa Uzunguni kata ya Kilimani.

“Kesho saa sita mchana tutapeleka mwili wa mpendwa wetu Kanisa la Mtakatifu Paul wa Msalaba na ibada itafanyika pale kisha msafara utaelekea Chizomoche kwa ajili ya mazishi,” amesema.

Baadhi ya viongozi waliofika nyumbani kwa marehemu ni mawaziri wakuu wastaafu Mizengo Pinda na John Malecela. Viongozi wengine wastaafu ni Balozi Job Lusinde, Joseph Butiku, William Kusila na Hezekia Chibulunje.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post