RAIS MAGUFULI ALIVYOPANGUA KAULI YA MNYIKA KUHUSU DEMOKRASIA NA VYUMA KUKAZA

Rais John Magufuli amemjibu mbunge wa Kibamba (Chadema), John Mnyika baada ya mbunge huyo kuhoji kuhusu demokrasia, vyuma kukaza na kuomba waliovunjiwa nyumba zao kupisha upanuzi wa barabara ya Morogoro kulipwa fidia.

Magufuli alitoa kauli hiyo jana Jumatano Desemba 19, 2018 muda mfupi kabla ya kuweka jiwe la msingi la upanuzi wa barabara ya Morogoro jijini Dar es Salaam katika eneo la Kimara Stop Over.

“Nilitegemea atakaposimama hapa angesema asanteni sana CCM, demokrasia ya namna gani anaitaka, hata kufunika midomo usiongee nayo ni demokrasia. Demokrasia siyo fujo, watu wafanye fujo mitaani wabomoe maduka halafu tuwaache eti kisa ni demokrasia? Haiwezekani. Demokaria ya kweli imehamia bungeni.

“Napenda kuwaambia ndugu zangu wa eneo hili la Kimara kuwa, ukivamia sehemu ya barabara ujue kabisa umetafuta umaskini, hivyo anayewaambia kua kuna fidia, mimi ninawaambia fidia haipo, narudia tena fidia haipo, fidia haipo.

Awali Mnyika alimuomba Rais Magufuli kuwalipa fidia wananchi waliyobomolewa nyumba zao katika eneo la Kimara kupisha upanuzi wa barabara hiyo, lakini Rais amesisitiza kuwa serikali haitalipa fidia kwa watu waliobomolewa nyumba zao kwa kuwa walikuwa wamejenga ndani ya hifadhi ya barabara.

“Wapo wanasema vyuma vimekaza, vitakaza kweli, asiyefanya kazi na asile, lazima tuwaambie ukweli hii ya vyuma vimekaza ni watu wanazushazusha. Wananchi wa Ubungo muache kulalamika vyuma vimekaza, mkatafute kazi ya hata ya kuchimba mtaro hivyo vyuma havitabana.

“Ninawaomba Watanzania wote, hebu tujiamni basi angalau kwa miaka mitano, nikishaondoka muache kujiamini, mfanye mnavyotaka. Kwa nchi inayojitambua hatuwezi kusubiri misaada, mtaji wa maskini ni nguvu zake mwenyewe, nchi hii sio katili. 

"Tuheshimu Sheria zetu, nafahamu Sheria ni ngumu na ndiyo maana unakuta hata sheria za Mussa hatuziheshimu, usitamani mwanamke wa mtu unakuta kila mtu anatamani tu.

“Kuna watu wanasema eti ni kodi zetu, kwani zamani mlikuwa hamlipi kodi? Mmbona hazikujengwa? Kwa nini msiseme tu kuwa ni juhudi za Rais Magufuli?. 

"Watu wamefariki kwa kushindwa kuwahi Muhimbili kwa ajili ya msongamano wa barabara hii, ndoa zimevunjika mtu anatumia sababu ya msongamano anarudi nyumbani usiku kumbe alikuwa pembeni anasema msongamano kumbe jamaa analiwa,” alisema Magufuli.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post