SAED KUBENEA : SINA MPANGO WA KUHAMIA CCM..MAKONDA ATAONDOKA KWA AIBU

Mbunge wa Ubungo (CHADEMA) Saed Kubenea amesema kuwa kitendo cha Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda kusema kuwa yeye na Mbunge wa Kibamba John Mnyika walitaka kujiunga na CCM, si kweli.

Kubenea amesema kuwa hawakuongea vile na Rais bali walikuwa wakizungumza mambo mengine, na Makonda amesema yale ili kuwafurahisha wanachama wa chama cha mapinduzi waliokuwepo kwenye hafla ile.

Kubenea amesema kuwa uchaguzi ujao watahakikisha kuwa wanashinda kwa kishindo hadi serikali inayoongozwa na CCM ishangae.

"Nataka nimwambie tu RC Makonda kwamba katika uchaguzi unaokuja upinzani tutashinda zaidi kuliko ilivyo kawaida, na ataondoka kwa aibu", amesema Kubenea.

Kubenea ameongeza, "Nchi yetu inajenga matabaka, mtu akionekana anaikosoa serikali wanasema huyu mpinzani na siku hizi wametupatia jina jipya wanatuita mawakala wa mabeberu".

Kubenea amesema kuwa, wale wanaomuunga mkono Rais Magufuli wengi wao ndio wanaompinga kimya kimya wakishirikiana na wanachama wengine ndani ya chama ambao wanajiandaa kumpinga katika uchaguzi ujao.

Hayo yamejiri baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda, kudai kuwa, amepokea maombi ya wanachama mbalimbali wanaotaka kujiunga na CCM, wakiwemo wabunge wawili wa CHADEMA, Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea na wa Kibamba, John Mnyika, wakati akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa uwekaji jiwe la msingi la ujenzi wa daraja la kisasa la Selander na barabara unganishi jijini Dar es salaam.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527