WAZIRI AWAPIGA MARUFUKU TRA KUFUNGIA BIASHARA ZA WADAIWA KODI

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amepiga marufuku Mamlaka ya Mapato nchini TRA kuwafungia wafanyabiashara, biashara zao kwasababu ya madeni ya kodi wanayodaiwa.

Ametoa kauli hiyo jijini Dodoma  Desemba 30, 2018 wakati akitoa taarifa ya hali ya uchumi wa taifa na utekelezaji wa bajeti ya serikali kwa kipindi cha miezi sita katika mwaka wa fedha 2018/19.

"Ninaukumbusha uongozi wa Mamlaka ya Mapato utekeleze maagizo ya Mhe Rais aliyoyatoa wakati wa ufunguzi wa kikao cha utendaji kazi wa mamlaka kilichofanyika ukumbi wa Mwl Nyerere tarehe 10 Desemba 2018," amesema.

"Utaratibu wa kumfungia mfanyabiashara biashara yake ili kushinikiza alipe kodi anayodaiwa, usitishwe isipokuwa kwa mkwepaji sugu na kwa kibali cha Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania," ameongeza.

Pamoja na mambo mengine, Waziri Mpango amesema makusanyo ya ndani yameongezeka na kufikia shilingi trilioni 7.37 sawa na asilimia 88.9 huku mapato yatokanayo na kodi yakiwa ni trilioni 6.23 sawa na asilimia 88 ya lengo lililowekwa kwa kipindi hicho.

Waziri Dk Mpango pia amesema mapato yasiyo ya kodi yamevuka zaidi ya lengo na kufikia asilimia 121 kwa kukusanya bilioni 936.03 ambayo ni zaidi ya lengo la shilingi bilioni 775.36 huku mapato ya halmashauri yakifikia bilioni 203.8 ikitokana na kuimarishwa kwa mfumo wa ukusanyaji mapato wa serikali hasa kwa njia za kielektroniki.

Aidha Wziri Mpango ameitaka mamlaka ya mapato nchini TRA kuhakikisha inatoza kodi kwa mujibu wa sheria na kanuni zake na kuondoa manyanyaso kwa wafanyabiashara ili wahamasike kuchangia kodi
Chanzo:Eatv

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post