SERIKALI YA TANZANIA YAMFYEKELEA MBALI MAKONDA KUSAKA MASHOGA... NI MAWAZO YAKE TU


Serikali ya Tanzania imesema kampeni ya kuwasaka watu wanaojihusisha na vitendo vya ushoga inayoratibiwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ni mawazo yake na si msimamo wa Serikali.


“Wizara ya Mambo ya Nje kwa niaba ya Serikali inapenda kuwajulisha wananchi na jumuiya ya kimataifa kupitia vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi kuhusu masuala ya ushoga yaliyoongelewa na mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam,” imeeleza taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki iliyotolewa leo Jumapili Novemba 4, 2018.

“Serikali ya Tanzania ingependa kufafanua kwamba hayo ni mawazo yake (Makonda) na si msimamo wa Serikali.”

Katika taarifa hiyo, Serikali imekumbusha na kusisitiza kuwa itaendelea kuheshimu mikataba yote ya kimataifa inayohusu haki za binadamu ambayo imesaini na kuridhia.

“Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea na itaendelea kuheshimu na kulinda haki hizo kama zilivyo katika Katiba,” imesema taarifa hiyo.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari Oktoba 31, 2018, Makonda alitangaza kampeni ya kukabiliana na vitendo vya ushoga katika jiji la Dar es Salaam.

Siku hiyo Makonda aliunda kamati ya watu 15 kwa ajili ya kupambana na wanaojihusisha na ushoga, wanaotapeli wengine kwa kutumia mitandao wakijifanya ni viongozi maarufu nchini.

Alisema wapo baadhi ya watu wanaoingizwa katika dimbwi hilo bila kupenda huku baadhi yao wakiwa katika hali mbaya ambayo hawawezi kuimudu.

Alisema wapo baadhi walioingia katika dimbwi hilo kwa kubakwa na kudanganywa na kwamba amewaongeza watu wa ushauri nasaha waweze kuwasaidia kimawazo ili kuondokana na suala hilo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527