WABUNGE WA CHADEMA,CUF WASUSIA VIAPO VYA WABUNGE WA CCM

Wabunge wa Chadema na wa CUF upande wa katibu mkuu Maalim Seif wamesusia kushuhudia kiapo cha wabunge wanne wa CCM wakati wabunge hao walipokuwa wanaapishwa.


Mkutano wa Bunge umeanza leo asubuhi Jumanne Novemba 6, 2018 na kuongozwa na Spika Job Ndugai.


Mara baada ya kumaliza dua na wimbo wa Taifa, uliwadia wasaa wa kiapo kwa wabunge wanne waliokuwa upinzani ambao walijiuzulu na kuhamia CCM ambako waliibuka washindi.


Wakati wa shughuli hiyo ya kiapo, wabunge hao wa Chadema na CUF upande wa Maalim Seif hawakuwapo bungeni.


Aliyekuwa wa kwanza kuapishwa ni Julius Kalanga (Monduli), akafuatia Mwita Waitara (Ukonga), akaja Timotheo Mzava (Korogwe vijijini) aliyepita bila kupingwa akichukua nafasi ya marehemu Stephen Ngonyani ‘Majimarefu’ aliyefariki dunia.


Wa mwisho kuapishwa alikuwa Zuberi Kuchauka (Liwale) ambaye awali alikuwa mbunge kupitia CUF. Mara baada ya kumaliza kuapishwa, wabunge hao wa Chadema na CUF walirejea bungeni.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527