JINSI MADIWANI WA CHADEMA,CCM WALIVYOCHAPANA MAKONDE DAR

Katika hali isiyokuwa ya kawaida ngumi zilipigwa jana Oktoba 3, 2018 kwenye ukumbi wa Anatoglo uliopo Manispaa ya Ilala jijini Dar es salaam ambako kulikuwa na uchaguzi wa Naibu Meya.


Katika uchaguzi huo, Omar Kumbilamoto (CCM) alitangazwa mshindi kwa kura 27 dhidi ya kura 25 za Adam Rajabu (CUF) aliyepata kura 25 huku Mgombea Patrick Assenga (CHADEMA) akikosa kura hata 1.


Ngumi hizo zilimhusisha Diwani wa Tabata (Chadema) Patrick Assenga aliyechapana makonde na baadhi ya madiwani wa CCM katika Ukumbi huo baada kuwepo kwa sintofahamu wakati wa kutangazwa matokeo hayo ya uchaguzi huo


Ikumbukwe, Uchaguzi huo ulifanyika baada ya Kumbilamoto aliyekuwa naibu meya Ilala kwa tiketi ya CUF kujiuzulu na kuhamia CCM, akieleza ameshindwa kuwatumikia wananchi kutokana na chama chake kuwa na mgogoro wa uongozi.


Assenga alisema chanzo cha vurugu hizo ni baadhi ya kura kuharibika lakini mkurugenzi wa manispaa hiyo, Jumanne Shauri alipinga na kusema hakuna kura iliyoharibika.


“Mzozo ulianzia katika chumba cha majumuisho ya kura, nikiwa kama mwangalizi wa kura niliona baadhi ya kura zimeharibika na hazifai kwa mujibu wa uchaguzi, lakini Shauri na watu wengine walikataa.


“Niliamua kuzishikilia zile kura nne zilizoharibika baada kuona hivyo Shauri alitoka nje ya chumba na kuwaita polisi ambao walikuja kuninyang’anya zile kura na kunitoa nje ya chumba.”alisema Assenga.


Alisema baada ya kutolewa katika chumba hicho alikwenda kuzungumza na madiwani wenzake wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ndipo wajumbe wa CCM walipomfuata na kuanza kurushiana maneno, kisha kuanza kuchapana makonde.


Akizungumzia uchaguzi huo, mkurugenzi wa manispaa hiyo, Jumanne Shauri amesema ulikuwa wa haki na ulifuata taratibu zote na wajumbe walikuwa 52. CCM 26 na Ukawa kwa maana ya CUF na Chadema 26.


Amesema baada ya mchakato wa kuhesabu kura kukamilika, Kumbilamoto alipata kura 27 wakati Rajab Penza wa CUF akipata 25.


Hata hivyo, Shauri amekiri vurugu kutokea akidai zilisababishwa na Assenga lakini polisi walifanikiwa kumdhibiti.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527