MKONGE UNAVYOWEZA KUONGEZA PATO LA WANANCHI NA TAIFA


Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Katani Ltd (MD) Juma Shamte akizungumzia fursa za mkonge

Na Yusuph Mussa, Korogwe

MFUMO wa Wakulima wadogo wa Mkonge wa Kibiashara (SISO), umefungua fursa kwa wanavijiji, wafanyakazi na Watanzania wote kushiriki kwenye mnyororo wa thamani, kukuza uzalishaji na kuendeleza zao la mkonge.

Kwani matumizi ya mkonge yanaendelea
kupanuka na kuhitaji viwanda vingi zaidi kama ilivyoainishwa kwenye mpango mkakati wa sekta wa kuzalisha tani milioni moja ya singa (brashi) za mkonge. Mwaka huu 2018, Skimu ya SISO inatimiza miaka 20 tangu Kampuni ya Katani Ltd kuasisi mfumo huo.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake jana Oktoba 25, 2018 kwenye Jiji la Tanga, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Katani Ltd Juma Shamte, alisema Sekta ya Mkonge Tanzania ni kongwe kwa kuwa na mfumo wa masoko wa Kimataifa, uwezo mkubwa wa kutoa ajira na kuleta mapato ya ndani na kigeni kwa wingi kama zao la kibiashara. 

"Zao la Mkonge lina historia na sifa zote kuwa zao la mkakati la Taifa na kama nchi kuongoza kwenye soko la dunia. Septemba 25, mwaka huu, Waziri wa Kilimo Dkt. Charles Tizeba alikutana na wadau wa SISO hususani wakulima na Katani Ltd, kutatua tofauti zilizopo za utekelezaji wa makubaliano ya uendeshaji na mgao wa maslahi kwenye mauzo ya mkonge. Kutokana na kukua kwa SISO kumeleta umuhimu wa kushirikisha na kuunganisha 
zaidi wakulima kupitia vyama vyao katika mnyororo wa thamani wa mkonge kwa wakulima kushiriki kuanzia kwenye masoko, usimamizi na kuweka kumbukumbu. 

"Majukumu mengi toka huko nyuma yalikuwa yakibebwa na kutekelezwa na Katani Ltd zaidi kwa kutoa ruzuku, dhamana, mikopo na karadha kwa ajili ya wakulima kwa gharama au kupunguza faida kwa Kampuni. Hatua hizi za maboresho zitajibu changamoto za kuongeza ushiriki wa wakulima kwenye mauzo, usimamizi wa majukumu ya wakulima na kugharamia huduma wenyewe. Mwelekeo wa kuboresha changamoto ziliopo ni kukamilisha pembuzi yakinifu ya mgawanyo wa mapato ambayo imekuwa inafanyiwa kazi na mshauri kupata mfumo 
wa kugawana majukumu na mapato kwa asilimia kwa kuzingatia misingi ya SISO ya kuongeza thamani kwa pamoja na kuuza kwa pamoja", alisema Shamte. 

Alisema lengo la maboresho hayo ya mgawanyo wa mapato ni kuimarisha misingi ya kibiashara kati ya Wakulima na Katani Ltd kwa kuzingatia mifumo ya masoko na uendeshaji shamba ya kimkonge kwa namna moja ama nyingine. Na wamepata mafanikio, kwani tangu Kampuni ya Katani Ltd ilipoanza mwaka 1997 na wazawa wawekezaji 85 ambao pia ni wataalamu wa mkonge kwa kuweka nguvu zao pamoja za kiuchumi na kitaaluma kununua rasilimali ambazo leo ndiyo Kampuni ya Katani Ltd, mwaka 1998 ilikaribisha wakulima wengine kwenye kilimo cha kibiashara na mnyororo wa thamani wa mkonge.

Shamte alisema mwaka 1999 utekelezaji wa mfumo wa SISO ulianza kwa upandaji wa hekta 30 wa kaya 54 katika shamba la Mwelya. Hadi mwaka 2017 upandaji umeongezeka kufikia hekta 8,268 sawa na ekari 20,670 kwa kaya 1,267 za wakulima katika shamba la Magoma, Magunga, Hale, Ngombezi na Mwelya yenye jumla ya hekta 20,000 sawa na ekari 50,0000. Mashamba yote hayo yapo wilayani Korogwe.

"Uzalishaji wa singa umepanda kutoka tani 849 mwaka 2005 hadi tani 4,587 mwaka 2017 sawa na ongezeko la mara tano na nusu. Katani Ltd imetoa mikopo kwa wakulima yenye thamani ya sh. bilioni nane (8) kwa ajili ya kupanda na kutunza mkonge. Pamoja na hilo Katani Ltd imetoa ruzuku kwa miaka 13 kwa wakulima kutoka kwenye faida yake, kuhakikisha wakulima wanaimarika katika shughuli zao za kilimo.

"Mwaka 2005 wakulima walipata mapato ya sh. milioni 139 kwa mwaka mzima na mpaka kufika mwaka 2017, walipata mapato ya sh. bilioni 3.743 kwa mwaka. Wakulima wameweza kupata mapato ya jumla ya sh. bilioni 20 hadi kufika mwaka 2017. Wakulima wameweza kujenga nyumba bora za kisasa, kusomesha watoto shule, kutumia huduma za umeme, maji, mawasiliano, fedha na kumiliki vyombo vya usafiri wa binafsi pamoja na kupata huduma za afya na ustawi wa jamii. Kuna wakulima 870 ambao ni wanachama wa hiari wa NSSF (National 
Social Security Fund)",alisema Shamte.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527