MKONGE ULIVYONUFAISHA WANANCHI WA HALE, KOROGWE


Baadhi ya bidhaa zitokanazo na mkonge, kuanzia kamba za kawaida na kudu. Bidhaa hizi zinatengenezwa kwenye Kiwanda cha Tancord kilichopo Ngomeni, Wilaya ya Muheza mkoani Tanga chini ya Kampuni ya Katani Ltd.
Baadhi ya bidhaa zitokanazo na mkonge, kuanzia viti, meza, mikoba ya kike na kiume, busati na vikapu. Bidhaa hizi zinatengenezwa kwenye Kiwanda cha Tancord kilichopo Ngomeni, Wilaya ya Muheza mkoani Tanga chini ya Kampuni ya Katani Ltd. 


Na Yusuph Mussa, Korogwe


KUWEPO kwa Kiwanda cha Mkonge Hale chini ya Kampuni ya Katani Ltd kilchopo Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga kumeleta mafanikio kutokana na mzunguko wa fedha kuongezeka, lakini pia kumechangia biashara ya mji huo kukua.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na mwandishi wa habari hizi jana Oktoba 22, 2018 kwenye mji mdogo wa Hale, baadhi ya wakulima, na wanasiasa, walisema mkonge umekuwa ukilimwa na watu tofauti kwenye Shamba la Mkonge Hale katika mfumo wa Wakulima wa Mkonge (SISO) kwa miaka 20 sasa.

Hivyo mfumo huo umewasaidia wananchi wa kada mbalimbali kupata kipato, kwani malipo yanapofanyika kwa mkulima na mfanyakazi, mzunguko wa fedha unakuwa mkubwa, kwani watu mbalimbali wanaingia sokoni na kwenye maduka kutafuta mahitaji.

"Kuwepo kwa Kiwanda cha Mkonge Hale kumeleta mafanikio makubwa kwa wananchi kwa takribani miaka 20, kwani kwa vile kilimo hiki tumekitoa kuwa cha wawekezaji wakubwa wa kigeni (zamani makabaila) na kuwa kilimo cha wakulima wadogo kwa mfumo wa SISO, kila mtu sasa ananufaika na mkonge kwa vile mkulima anapata, mfanyakazi wa Katani Ltd anapata na mfanyabiashara anapata.

"Lakini tangu uzalishaji umesimama kwenye Kiwanda cha Mkonge Hale, mzunguko wa pesa umepungua," alisema Diwani wa Kata ya Hale Yusuph Nkondo.

Nkondo ambaye pia ni mkulima wa mkonge, alisema anaamini Serikali italichukulia kwa uzito mkubwa suala la kutafuta mgawanyo wa mapato kati ya wakulima na Katani Ltd haraka, ili shughuli za uzalishaji ziendelee, kwani kwa mkonge uliokomaa kuacha kuvunwa kwa miezi mitatu sasa, unaendelea kuharibika ukiwa shambani. Lakini hata wakulima, wafanyakazi na wananchi wanakosa mapato.

"Waziri wa Kilimo Dkt. Charles Tizeba alipofanya ziara ya kutembelea mashamba ya mkonge chini ya mfumo wa SISO Septemba 25, mwaka huu, alisema atalishughulikia suala la wakulima na Katani Ltd ndani ya siku 14, yaani hadi Oktoba 9, mwaka huu, lakini kama wakulima, bado hatujapata lolote kama tayari sisi tunapata kiasi gani cha mgawanyo wa mapato, na Katani Ltd watapata asilimia ngapi" ,alisema Nkondo.

Mkulima Maria Msindo wa Shamba la Mkonge Hale alisema kilimo cha mkonge kwake ni mkombozi, kwani ameweza kuendesha maisha yake kwa kupitia kilimo hicho. 

Chanzo cha kutafutwa muafaka wa maslahi na mgawanyo wa mapato, ni baada ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga kuunda Kamati ya kuchunguza madeni kati ya Kampuni ya Katani Ltd na wakulima wa mkonge kupitia mfumo wa SISO. Ni baada na yeye kupelekewa malalamiko na baadhi ya viongozi wa wakulima, hasa kutoka Shamba la Mkonge Mwelya, kuwa wanadai fedha Katani Ltd, lakini hawalipwi.

Lakini Katani Ltd nao wakidai wanadai fedha nyingi kutoka kwa wakulima baada ya kuwakopesha wakulima ili kuendeleza zao la mkonge, lakini hawalipi. Baada ya Kamati hiyo kuwasilisha taarifa yake mbele ya wadau wa mkonge Agosti 21, mwaka huu mjini Korogwe, ndipo Kamati ikaja na mapendekezo ambayo ndiyo yanafanyiwa kazi kwa sasa, huku viwanda hivyo vinane vya Katani Ltd vinavyohudumia wakulima kwa mfumo wa SISO kufungwa ili kupata kwanza muafaka.

Pamoja na Shigela kupita kwenye mashamba hayo baada ya Kamati kutoa mapendekezo yake ambayo baadae yaliwekewa maazimio, huku akiwashawishi wakulima kuendelea na uzalishaji muafaka kamili ukitafutwa, bado baadhi ya wakulima walikataa wakikataa mgawanyo wa mapato wa asilimia 54 kwa Katani Ltd na asilimia 46 kwa wakukima, ndipo Dkt. Tizeba alipokwenda kuonana na wakulima hao, na kuahidi kushughulikia jambo hilo ndani ya siku 14.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post