WAKULIMA WAELEZA KATANI LTD ILIVYOWASAIDIA

Na Yusuph Mussa, Korogwe

BAADHI ya wafanyakazi wa Kampuni ya Katani Ltd, Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga, wameishukuru kampuni hiyo kwa kuwafanya waendelee kupata ajira na kuendesha maisha yao, kwa madai baada ya mashirika ya mkonge kufa miaka ya 1990 hawakujua wafanye nini.

Ni baada ya baadhi yao kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania, ambapo walishindwa kurudi huko kutokana na kukabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kubaki kwenye makambi ya mkonge bila kulipwa mafao yao mara baada ya mashirika hayo kufa.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi Oktoba 15, 2018 kwa nyakati tofauti kwenye Shamba la Mkonge Ngombezi, walisema baada ya Serikali ya Awamu ya Tatu kubinafsisha mashirika mufilisi, ndipo Kampuni ya Katani Ltd iliponunua mashamba matano ya mkonge wilayani Korogwe ya Hale, Ngombezi, Mwelya, Magoma na Magunga.

Wafanyakazi wa Katani Ltd na wakulima wa mkonge kupitia mfumo wa SISO (Wakulima wa Mkonge), waliyasema hayo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 20 ya Kampuni ya Katani Ltd.

"Tunashukuru kwa kuwepo kampuni ya Katani Ltd, imetusaidia kuendelea kubaki mkoa wa Tanga. Mimi kwetu Songea (mkoani Ruvuma) kwa kweli nisingeweza kurudi huko kutokana na matatizo tuliyokuwa nayo wakati huo hasa kwa kushindwa kulipwa mafao yetu sisi tuliokuwa wafanyakazi kwenye mkonge" alisena Green Wikika mfanyakazi wa Kiwanda cha Mkonge Ngombezi ambacho kipo chini ya Katani Ltd.

Wikika pamoja na kuwa mfanyakazi, lakini pia ni mkulima wa mkonge, amesema kwa sasa mapato ya mkonge yamepungua tofauti wakati wanaanza mfumo wa SISO, kwani walikuwa wanauza meta (mzigo wa majani ya mkonge) na sasa wanauza singa (brashi), hivyo amewataka wadau kuona maslahi ya wakulima kupitia mfumo wa SISO yanaboreshwa.

Wikika alisema kufungwa viwanda vinane (8) vya mkonge vilivyo chini ya Katani Ltd kwa sasa kunawaathiri, lakini kwa vile suala hilo tayari Mkuu wa Mkoa wa Tanga Martin Shigela ameshaingilia kati, na sasa hivi unatafutwa muafaka wa kimaslahi kati ya Katani Ltd na wakulima, wanaendelea kusubiri.

"Sasa hivi hapa hapa kwetu Ngombezi, baada ya kiwanda kufungwa, kuna wanaume wameshakimbia wake zao na watoto wao kwa kisingizio cha kwenda kutafuta kazi kwenye mashamba mengine ya mkonge" alisema Wikika.

Mkulima wa mkonge Shamba la Ngombezi Damas Katabanya alisema kwa kiwango kikubwa Katani Ltd imewafanya waweze kuendesha maisha yao kwa kile wanachopata kila wakiuza mkonge, hivyo umefika wakati Serikali iwasaidie kwa kutatua matatizo yao mapema ili maisha yaendelee.

Mkulima mwingine wa mkonge Shamba la Ngombezi John Magenza kutoka Kasulu mkoani Kigoma, alisema tangu uzalishaji umesimama zaidi ya miezi miwili sasa, wameshindwa kutuma nauli ili waweze kuungana na familia zao kutokana na kushindwa kupata fedha.

Mfanyakazi wa Katani Ltd Kiwanda cha Ngombezi ambaye yupo idara ya upishi, Prisca Deo, alisema anaiomba kampuni hiyo imsaidie kuweza kumpeleka mtoto wake kwenda kuanza masomo Chuo cha Ualimu Kigoma.

"Mimi nina shida, na nilifika ofisini kumlalamikia Meneja wa Ngombezi Bryceson Urio kuwa mtoto wangu anatakiwa kwenda Chuo cha Ualimu Kigoma. Sio huyo tu, hata mhasibu wa Katani Mhina alipita nyumbani kwangu, nikamueleza suala hilo, wananieleza niendelee kusubiri, lakini hadi sasa bado" alisema Deo.

Akizungumza na mwandishi, Urio alikiri mama huyo kufika ofisini kwake akiwa analia, lakini hawana jinsi. Pamoja na changamoto zilizopo, ili kuwalipa wafanyakazi ni lazima kuwe na uzalishaji, hivyo wanasubiri Serikali ikamilishe kazi yake.
Mkonge ukisubiri kuingizwa kwenye PRESS (Mashine ya kufunga robota) katika Kiwanda cha Mkonge Ngombezi. (Picha na Yusuph Mussa).
Sehemu ya Jengo la Makao Makuu ya Kampuni ya Katani Ltd yaliyopo Jiji la Tanga. (Picha na Yusuph Mussa).
Mfanyakazi wa Kampuni ya Katani Ltd, Kiwanda cha Ngombezi Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga, Prisca Deo, akielezea namna anavyoathirika kwa kukosa mshahara baada ya kiwanda hicho kufungwa kwa zaidi ya miezi miwili sasa kwa ajili ya kutafuta muafaka wa maslahi ya wakulima na kampuni hiyo. Amedai mtoto wake anatakiwa kwenda Chuo cha Ualimu mkoani Kigoma, lakini ameshindwa kufanya hivyo. (Picha na Yusuph Mussa).
Mfanyakazi na mkulima wa Kampuni ya Katani Ltd, Kiwanda cha Ngombezi Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga, Green Wikika, akielezea namna alivyonufaika baada ya Kampuni ya Katani Ltd ilivyoamua kununua mashamba ya mkonge mwaka 1998, na wao kuendelea kupata ajira na kulima zao hilo. (Picha na Yusuph Mussa).

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post