DK BASHIRU AIKAANGA CCM YAKE KIAINA "USHINDI WA CCM UNAZIDI KUSHUKA...WAJANJA WANAONA KUPIGA KURA NI KITUKO

 Katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally amesema ushindi wa CCM unazidi kuporomoka siku hadi siku kutokana na wapigajikura kukosa imani na mifumo ya uchaguzi, ikiwa pamoja na vyama kutoa rushwa za mavazi na pesa.


Mbali na idadi ya wapigakura kupungua, Dk Bashiru amesema Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 ulizalisha Serikali isiyokuwa na uhalali wa kisiasa kwa kuwa watu wengi hawakujitokeza kupiga kura.

Dk Bashiru amesema hayo leo alipokuwa akitoa mada katika Kongamano la Mtandao wa Vikundi vya Wakulima (Mviwata) lililofanyika kwenye ukumbi wa Chuo Kikuu cha Waislamu Morogoro mjini Morogoro, ambako alieleza kwa kina jinsi idadi ya wapigakura inavyozidi kupungua kutokana na tabia za vyama na wanasiasa.

"Sasa wapigaji kura wajanja wa Tanzania wameanza tabia ya kudharau uchaguzi,” alisema Dk Bashiru mbele ya wakulima waliofurika kwenye ukumbi huo.

“(Wameanza tabia) Ya kukaa nyumbani kwa sababu wanaona ni kituko, ni mchezo wa kuigiza. Ndio maana leo kupata watu kwenda kupiga kura imekuwa shida. Note (angalia), tunakoshinda ni chini ya asilimia 30, chini ya asilimia 40. Hakuna mahali ambako wapigajikura wamejitokeza kwa asilimia 50," alisema Dk Bashiru.

"Na mwaka 2010 ulitia fora. Watu wengi walijiandikisha, kumbe walikuwa wanataka kile kiparata (kitambulisho cha mpigakura), kwa sababu kinatumika kwenda polisi kudhamini, kujitambulisha.

“Walipokipata wakaingia mitini. Kwa Mara ya kwanza katika historia ya nchi hii tulipata Serikali ambayo haina uhalali wa kisiasa kwa sababu wapigajikura wengi zaidi ya asilimia 50 walibaki nyumbani. Tatizo hili halijaisha, lakini wanasiasa wakishashinda, wanasema ameshinda hata kama ni kura moja. Hajali kwamba ushindi ule unatakiwa uwe na uhalali."

Alisema mfumo wa uchaguzi nchini umegubikwa na rushwa kiasi kwamba imefika mahali ambapo ukifika uchaguzi wagombea wanauza nyumba.

“Usipomchangia, anakuwa mkali utafikiri anakwenda kutibiwa,” alisema.

"Akishazikusanya fedha anakwenda kuwanunua wale mawakala na mawakala wanajua. Nao wanawanunua wapigaji kura. Msimu wa uchaguzi unakuwa msimu wa rushwa ya uchaguzi. Mnachotakiwa kufanya ni kubomoa na kuharibu soko la kura."


Via>>Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527