MWANAUME ANAYEBAKA WANAWAKE ADAKWA MWANZA


Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza.

Jeshi la polisi mkoa wa Mwanza linawashikilia watu watatu ambao wamekuwa wakifanya vitendo vya kihalifu katika maeneo mbalimbali mkoani humo, akiwemo mtuhumiwa wa tukio la ubakaji.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jonathan Shanna, amemtaja mtuhumiwa huyo kuwa ni Kennedy Obworo, mwenye umri wa miaka 35, ambaye amekuwa akiwawekea wanawake dawa za kulevya katika vinywaji na kisha kuwabaka na kuwaibia vitu walivyonavyo.

Katika tukio jingine, jeshi hilo linamshikilia Sheshe Mazoya, anayedaiwa kuwa mganga wa kienyeji mkazi wa Wilaya ya Magu kwa kosa la kukutwa na nyara mbalimbali za serikali ikiwemo mikia miwili ya nyumbu na pembe moja ya swala, kucha za Simba na miiba ya nungunungu ambavyo alikuwa anavimiliki kinyume na sheria.

Aidha, Kamanda Shanna amesema wanamshikilia mwanamke anayefahamika kwa jina la Sonia Fanuel kwa kosa la wizi wa kufungua milango kwa kutumia funguo bandia.

Kamanda Shanna ambaye amechukua nafasi ya Kamanda Ahmed Msangi aliyehamishiwa makao makuu, amesema watuhumiwa wote wanatarajiwa kufikishwa Mahakamani Jumatatu ijayo kujibu tuhuma zinazowakabili.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527