MUME AMUUA MKE WAKE KWA KUMKATA MAPANGA


Mwanamke mmoja mkazi wa kijiji cha Pangaro, wilaya ya Mwanga, Kilimanjaro, Ziada Mwalimu (46) amefariki dunia akidaiwa kukatwakatwa mapanga kichwani na mikononi na mume wake.

Tukio hilo limetokea Septemba 7 mwaka huu linadaiwa kusababishwa na migogoro ya kifamilia baina ya marehemu na mume wake aliyefahamika kwa jina la Abdi Shabani (37)

Akitoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari leo Septemba 11 mjini Moshi, kamanda wa polisi mkoani Kilimanjaro, Hamis Issah amesema mauaji hayo ya kikatili yametokea saa 2:00 usiku katika kijiji hicho.

Akielezea mazingira ya tukio hilo, Kamanda Issah amesema kuwa mshtakiwa alitenda ukatili huo wakiwa nyumbani kwao na inaelezwa kuwa alikuwa akimtuhumu mkewe kuwa hampendi na haipendi familia yake.

“Chanzo cha tukio hilo ni mgogoro wa kifamilia waliokuwa nao watu hawa,"amesema Kamanda Issah.

Kwa mujibu wa kamanda Issah, baada ya mwanaume huyo kufanya mauaji hayo alikimbia lakini jeshi la polisi lilipata taarifa na kuanza kumsaka na walifanikiwa kumkamata.

"Mtuhumiwa alipohojiwa, alidai kuwa mke wake alikuwa hampendi pamoja na familia yao hali iliyosababisha wajengewe kinyumba pembeni jambo lililomchukiza na kuamua afanye mauaji hayo,"amesema.

Kamanda amesema taratibu za kumfikisha mahakamani zinaendelea.


Na Florah Temba, Mwananchi.

Download/Pakua App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527