MWANAFUNZI WA KIDATO CHA NNE AJIUA BAADA YA KUHOJIWA NA WALIMU TUHUMA ZA MAPENZI


Mwanafunzi wa kidato cha nne katika shule ya sekondari ya Rau iliyopo katika manispaa ya Moshi,mkoani Kilimanjaro Emmanuel Tarimo (18), amejinyonga hadi kufa baada ya kudaiwa kuhojiwa na walimu wake kwa zaidi ya saa tano, akituhumiwa kujihusisha kimapenzi na mwanafunzi mwenzake wa kidato cha kwanza.

Kamanda wa polisi mkoa wa Kilimanjaro, ACP Hamis Issa amethibitisha kutokea kwa tukio hilo kati ya majira ya saa nne za usiku nyumbani kwao mtaa wa Sababa, Rau Madukani, manispaa ya Moshi.

Sababu inayotajwa kusababisha kifo cha mwanafunzi huyo ambaye anajiandaa kufanya mitihani ya kuhitimu kidato cha nne mwaka huu ni kuhusishwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanafunzi mwenzake katika moja ya ofisi ya walimu iliyokuwa wazi shuleni hapo.

Mkuu wa shule ya sekondari Rau Bw.Nyoni Njinjinji amekiri mwanafunzi huyo kuhojiwa na walimu kuhusiana na tuhuma za kujihusisha kimapenzi na mwenzake ambapo baada ya kukataa, alielekezwa kujieleza kwa barua na alipomaliza aliondoka na kuelekea nyumbani badala ya kuingia darasani.

Kwa upande wake mama mdogo wa marehemu Bi. Teddy Maro na baadhi ya wanafunzi kwa nyakati tofauti ,wameeleza kusikitishwa kwao na kifo cha mwanafunzi huyo,huku wakiwasihi walimu kutojenga tabia ya kuwasukuma wanafunzi kukiri kosa ambalo huenda linaweza kuwa si kweli na likawaathiri kisaikolojia.
Chanzo- ITV

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527