NAPE NNAUYE APONDA KIAINA HAMAHAMA YA WABUNGE NA MADIWANI..ATAKA THAMANI YA WAPIGA KURA ITHAMINIWE



Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye amesema ipo haja ya kupitiwa upya kwa sheria inayosimamia thamani ya kura hasa katika kipindi hiki cha wabunge na madiwani kuhama vyama vyao.

Ametoa kauli hiyo jana Alhamisi Agosti 16, 2018 katika ofisi ndogo za Bunge visiwani Zanzibar katika mafunzo ya siku mbili ya kamati ya uongozi, makamu wenyeviti wa kamati za Bunge pamoja na wajumbe wa tume ya utumishi wa Bunge.

Amesema pamoja na uwepo wa wimbi kubwa la wanasiasa kuhama, wapigakura wanatakiwa kupewa thamani yao kwa kuwa wakati wa uchaguzi wao ndio uhitajika kupiga kura kuchagua wawakilishi wao.

Amebainisha kuwa licha ya Katiba ya nchi na sheria mbalimbali kutominya fursa ya mwanasiasa kuhama chama kimoja na kwenda kingine, bado thamani ya mpiga kura inapaswa kuenziwa.

"Siwezi kupingana na Katiba kuhusu hamahama za wanasiasa lakini ni vyema thamani za wapiga kura ikatambulika vyema,” amesema Nape.

Katibu huyo wa zamani wa Itikadi na Uenezi wa CCM, amesema ni vyema kukawa na sheria ambayo itampa mamlaka mbunge au diwani anayehama chama baada ya uchaguzi, aendelee kuwa na nafasi hizo katika chama anachokwenda.

Amesema jambo hilo likifanyika litaokoa kiasi kikubwa cha fedha kinachotumika katika chaguzi ndogo kwenye maeneo ambayo mbunge au diwani amehamia chama kingine.
Na Haji Mtumwa,Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527