NAIBU MEYA ILALA AJIUZULU

Diwani wa Kata ya Vingunguti (CUF), Omary Kumbilamoto ambaye pia ni naibu meya wa manispaa ya Ilala amejizulu uanachama wa chama hicho.


Amechukua uamuzi huo jana Julai 31, 2018 huku akieleza kuchoshwa na mgogoro wa uongozi unaoendelea ndani ya CUF.


CUF kimekumbwa na mgogoro tangu mwaka 2016 baada ya kurejea kwa Profesa Ibrahim Lipumba ambaye mwaka 2015 alijiuzulu uenyekiti wa chama hicho kutokana na kutofautiana na viongozi wenzake.


Kumbilamoto ameufananisha mgogoro huo wa CUF na mvutano wa mataifa ya Palestina na Israel, akieleza kuwa hauna suluhu na unamfanya ashindwe kuwatumikia ipasavyo wananchi wa Vingunguti.


Amesema amekuwa akipewa vitisho vya kufukuzwa uanachama kwa sababu ya hatua yake ya kuwa karibu na viongozi wa Serikali akiwamo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.


Amesema wakati kata ya Vingunguti ikikumbwa na mafuriko, hakuna kiongozi yoyote wa CUF aliyekwenda kutoa msaada isipokuwa Serikali ya Mkoa wa Dar es Salaam.


“Sikuletewa hata kijiko na viongozi wangu wa chama lakini viongozi wa Serikali walinisaidia. Hata hivyo, upande chama kinadai mimi ni msaliti kutokana na ushirikiano ninaoupata,” amesema Kumbilamoto.


Amesema wakati wowote atafanya mkutano wa hadhara wa kueleza wa wananchi wa kata hiyo wapi atakapoelekea kwa ajili ya kufanya shughuli za kisiasa.


Credit: Mwananchi
Theme images by rion819. Powered by Blogger.