DADA WA RAIS MAGUFULI AFARIKI DUNIA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli alipoenda kumjulia hali Dada yake Monica Joseph Magufuli ambaye alikuwa amelazwa katika Chumba cha uangalizi Maalum ICU katika hospitali ya Bugando mkoani Mwanza.

***
Aliyekuwa dada wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli, Bi. Monica Joseph Magufuli amefariki dunia asubuhi ya leo Agosti 19, 2018 katika hospitali ya Bugando Jijini Mwanza alikokuwa anapatiwa matibabu.

Jana Jumamosi Rais Magufuli alimtembelea dada yake kumjulia hali akiwa amelazwa chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum ICU, ambapo Rais Magufuli alisikika akiwaambia madaktari na wauguzi wa hospitali hiyo kwamba, hali ya dada yake ni mbaya.

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa ametoa taarifa za msiba huo kupitia mitandao ya kijamii ambapo ameandika, “Nasikitika kuwajulisha kuwa Dada wa Rais (John Magufuli) Monica Joseph Magufuli amefariki dunia asubuhi leo Agosti 19, 2018 katika hospitali ya Bugando jijini Mwanza alikokuwa akipatiwa matibabu,”.

Monica amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 63 (alizaliwa tarehe 25 Novemba, 1955) na ameacha watoto 9 na wajukuu 25.
Theme images by rion819. Powered by Blogger.