GARI LA MSHINDI 'MISS LAKE ZONE 2018' LAKATALIWA


Gari aina ya Passo lililoandaliwa kwa ajili ya zawadi ya atakayeibuka mshindi wa Miss Lake Zone 

Gari lililozua gumzo mitandaoni ambalo angekabidhiwa mshindi wa Miss Lake Zone katika fainali za mashindano hayo zitakazofanyika kesho jijini Mwanza, limekataliwa na waandaaji wa Miss Tanzania.

Tayari waandaaji hao wa Miss Lake Zone wameandikiwa barua wakitakiwa kutafuta zawadi nyingine.

Akizungumza na MCL Digital leo Ijumaa Agosti 3, 2018, mkurugenzi wa The Look Company inayoandaa Miss Tanzania, Basilla Mwanukuzi amesema wamewaandikia barua waandaaji na kutuma nakala Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), wakiwataka wabadilishe zawadi hiyo na kutoa inayoendana na mashindano.

“Zawadi hiyo haiendani na hadhi ya mashindano, najua wanajitahidi kutoa zawadi kubwa lakini kusema ukweli hatujaafiki, tumejaribu kuwapigia simu kuwaeleza lakini hawapokei, sasa tumewaandikia barua na nakala tumetuma Basata, “ amesema Basilla.

Amesema waandaaji wa ngazi ya chini hawana ulazima wa kutoa zawadi kubwa bali kuwatafuta wasichana wenye vigezo na kuendesha mashindano kwa weledi.

“Zawadi kubwa za magari inabidi watuachie sisi huku juu na siyo kulazimisha, ninajua wana nia njema lakini hili hatukubaliani nalo,” amefafanua.

Mwandaaji wa mashindano hayo, Fred Kikoti amesema hana taarifa yoyote ya kukataliwa zawadi hiyo ya gari aina ya Passo lenye thamani ya Sh8 milioni.

“Fainali za mashindano ni kesho na tunaendelea vyema, kuhusu waratibu wa Miss Tanzania bado hatuna mawasiliano yoyote lakini tunajua watafika tu kwa sababu na wenyewe ni sehemu ya majaji watakaokuwepo kesho,” amesema Kikoti.

Jumla ya warembo 15 watachuana kesho Jumamosi Agosti 4, 2018 katika fainali na mashindano hayo ambayo sasa mshindi inabidi atafutiwe zawadi nyingine.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527