LIPUMBA AMTAKA MAALIM SEIF KUFUTA KESI ZISIZO NA MASHIKO MAHAKAMANI


Mwenyekiti wa CUF anayetambuliwa na msajili wa vyama vya siasa nchini, Profesa Ibrahim Lipumba (kulia) akiwa na Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad.

Mwenyekiti wa CUF anayetambuliwa na msajili wa vyama vya siasa nchini, Profesa Ibrahim Lipumba amemtaka Maalim Seif Sharif Hamad kufuta kesi zisizo na mashiko walizofungua mahakamani ili kuepukana na hasara ambazo zinaweza kuepukika.

Lipumba amesema si jambo la busara hata kidogo kwa wakati huu ambao nchi ipo katika kipindi cha amani na utulivu kundi la watu likaibuka na kuanza kufungua kesi za kisiasa ambazo kuwepo kwake ni kupoteza muda kwa kundi lililofungua kesi hizo.

Lipumba ametoa kauli hiyo janaAgosti 16,2018 katika mkutano na waandishi na habari huko Malindi Mjini Unguja, wenye lengo la kutoa msimamo wa chama chake juu ya ushiriki wao katika chaguzi ndogo ndogo za wabunge na wawakilishi, ambapo amesema kuwa chama hicho kitashiriki katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Jang'ombe utakaofanyika Desemba mwaka huu.

"Hatuwezi kuwaachia fursa ya kushiriki uchaguzi mdogo kwa kisingizio cha mgongano uliopo baina yetu, sisi lengo letu ni kutumikia wananchi hivyo tunaahidi kuwa tutashiriki uchaguzi bila ya wasi wasi wowote,"amesema Lipumba.

Lipumba ameongeza kuwa, "Niwaombe sana ndugu zangu akina Maalim Seif kufuta kesi zao Mahakamani kwani kinyume chake wataendelea kuwanufaisha mawakili tu wala hakutakuwa na jambo jipya juu ya kesi hizo".

Amesema kwa kuwa CUF ni sehemu ya vyama vya siasa ambavyo vina haki ya kushiriki uchaguzi huo wa marejeo hivyo ni wazi kuwa hawataacha kushiriki uchaguzi ili kuwapa fursa wananchi kukichagua chao hicho ili kuwatumikia .

Kwa zaidi ya miaka miwili sasa, Chama cha Wananchi (CUF) kipo kwenye mgogoro mkubwa wa kiutawala uliosababishwa na hatua ya Profesa Ibrahimu Lipumba kujiuzulu na baadaye kutengua uamuzi huo.

Profesa Lipumba alitangaza kujiuzulu uenyekiti, Agosti 5, 2015 lakini baada ya mwaka mmoja akatengua uamuzi huo na kutangaza kurejea katika wadhifa huo jambo ambalo limepingwa na baadhi ya wanachama wakiongozwa na Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527