KOCHA : SIJAMSAJILI ALIKIBA SABABU YA KUIMBA SANA


Juma Mgunda (kushoto) na Alikiba (kulia).

Kocha mkuu wa klabu ya Coastal Union ya Tanga, Juma Mgunda, amefunguka juu ya kiwango cha mchezaji mpya wa klabu hiyo, AliKiba katika mazoezi yake ya kwanza tangu ajiunge nayo msimu huu.

Alikiba yupo mkoani Tanga na Ijumaa, Agosti 3, amehudhuria mazoezi ya klabu hiyo ikiwa ni katika maandalizi ya msimu mpya wa ligi kuu Tanzania bara unaotarajia kutimua vumbi, Agosti 22.

Akizungumza mara baada ya kukamilika kwa programu ya mazoezi hayo, kocha Mgunda amesema .

“ Alikiba mimi nimemsajili kwasababu nimemwona anajua kucheza na wala sikumsajili Ali kwasababu anaimba sana, kwahiyo nataka ule uwezo wake wa kucheza ndiyo maana nikazungumza naye nikamshawishi akaniambia mwalimu nitafikiria na kweli akafikiria akaniambia niko tayari kucheza “.

Pia amewataka mashabiki wa Coastal Union na wadau wa soka nchini kuondoa wasiwasi juu ya mchezaji huyo na kwamba wategemee mambo mazuri kutoka kwake.

Coastal Union imeingia mkataba wa mwaka mmoja na Alikiba, mkataba ambao unamruhusu kufanya kazi yake ya awali ya kimuziki kama kawaida na kuruhusiwa kucheza pale anakuwa hana majukumu mazito.

Klabu hiyo iliyopanda ligi kuu msimu huu baada ya kushiriki kwa mara ya mwisho msimu wa 2015/16, itaanza kampeni ya ligi kuu Tanzania bara, Agosti 22 itakapowakaribisha ‘Wanapalohengo’ Lipuli Fc ya mkoani Iringa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527