CHADEMA WAIANDIKIA BARUA TUME YA TAIFA YA UCHAGUZ KUPINGA MGOMBEA WAO KUENGULIWA KOROGWE VIJIJINI

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeiandikia barua Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kikilalamikia kile kilichotokea Korogwe Vijijini.

Barua hiyo imeandikwa na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji jana jioni Augusti 21, 2018 imekwenda kwa Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Dk Athuman Kihamia na msimamizi wa uchaguzi jimbo la Korogwe Vijijini, Dk George Nyaronga.

Barua hiyo ya Dk Mashinji kwenda kwa Dk Kihamia aliituma baada ya Dk Nyaronga kumtangaza mgombea wa CCM, Timotheo Mzava kupita bila kupingwa.

Katika barua hiyo yenye kumbukumbu namba C/HQ/ADM/TU/05/80, nakala yake imetumwa kwa Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Semistocles Kaijage, msimamizi wa uchaguzi Korogwe Vijijini, Dk Nyaronga.

“Rejea mazungumzo yetu ya simu awali leo (jana) saa 6:03 mchana na ukanirudia saa 06:06 kuhusu msimamizi wa uchaguzi Korogwe kutopokea fomu ya mgombea ubunge kupitia Chadema, Amina Ally Saguti ambaye alikuwapo muda wote leo (jana) kuanzia saa 4:00 asubuhi ofisi ya msimamizi wa uchaguzi wa jimbo la Korogwe Vijijini, jambo ambalo uliahidi kulighulikia,” anasema Dk Mashinji.

“Nilikurejea tena saa 09:47 jioni kukujulisha kuwa bado msimamizi wa uchaguzi wa jimbo la Korogwe Vijijini hajapokea fomu za mgombea kupitia Chadema na ukanirejea tena saa 09:55 ukinieleza kuwa unashughulikia.”

Katika barua hiyo, Dk Mashinji anasema: “Katika mazingira hayo, tunaitaka ofisi yako na Tume iingilie kati suala hili kubwa la uvunjifu wa sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi ili mchakato urejewe kuruhusu mgombea wetu wa Chadema na wengine waliochukua fomu za uteuzi waweze kurejesha fomu hizo kwa ajili ya uteuzi.”

“Pamoja na kuingilia suala hili, tunaitaka pia ofisi yako iitishe mara moja kikao cha maadili cha Taifa kwa ajili ya kumjadili msimamizi wa uchaguzi wa jimbo la Korogwe Vijijini na OCD (mkuu wa polisi wilaya) wa Korogwe ili hatua kali za nidhamu zichukuliwe dhidi yao na wote wanaohusika,” amesema Dk Maashinji

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527