WANANCHI WENYE HASIRA WACHOMA MOTO NYUMBA MBILI MWANZA

Kwamba tarehe 25.07.2018 majira ya saa 03:00hrs usiku katika mtaa wa Nyakabungo “A” kata ya Isamilo wilaya ya Nyamgana jiji na mkoa wa Mwanza, nyumba mbili mali ya Selina Francis, @ mama Mkapa, miaka 50, mkazi wa mtaa Nyakabungo na Abdalah Mwita @ Machela, zimechomwa moto na kundi la wananchi waliojichukulia sheria mkononi baada ya kuona watoto wa wahanga tajwa hapo juu wakijihusisha na uhalifu hapo mtaani mara kwa mara kwani watoto hao wamekuwa wakikamatwa na kufikishwa mahakamani lakini wamekua wakiachiliwa kwa dhamana kisha kurudia tena kutenda uhalifu kitendo ambacho kimekuwa kero kubwa kwa wananchi wa eneo hilo.


Vilevile nyumba moja mali ya Manka Francis James @Mushi, iliharibiwa vibaya na kundi hilo la wananchi kwa kuvunjwa milango na madirisha na kuharibiwa vitu mbalimbali vilivyokuwemo ndani kwa kumtuhumu mwanamke huyo kuwa anashiriki katika kuficha wezi na vibaka pamoja na kujihusisha na utapeli kwa wananchi wa mtaani hapo na Mwanza kwa ujumla kwa kuwauzia dhahabu bandia, kitendo ambacho ni kosa kisheria.


Inadaiwa kuwa wananchi wa mtaa tajwa hapo juu wamekuwa wakimlalamikia na kumtuhumu mtoto wa Mama Selina Francis aitwaye Mkapa Mwabe pamoja na mtoto wa mzee Abdalah Mwita aitwaye Emmanuel Mwita @ Mwita kuwa ni wezi/vibaka mtaani hapo. 


Vilevile wakimtuhumu Manka Fransis James @ Mushi kwa kushiriki kuwaficha wezi na vibaka nyumbani kwake pindi wanapotenda uhalifu mtaani na kuwatapeli wananchi kwa kuwauzia dhahabu feki.


Inasemekana kuwa kutokana na tuhuma hizo ndipo tarehe na majira tajwa hapo juu kundi la wananchi waliojawa na hasira kutokana na vitendo vya waanga walikwenda na kuvamia nyumba ya bwana Abdalah Mwita pamoja na nyumba ya mama Selina Francis ambapo waliwakuta watoto wadogo, wenye nyumba hawakuwepo kisha waliwatoa watoto nje na kuchoma nyumba hizo moto. 


Aidha inadaiwa kuwa baada ya hapo kundi hilo la wananchi lilikwenda kwenye nyumba ya Manka Francis pia walikuta watoto mwenye nyumba hakuwepo kisha waliwatoa watoto nje na walivunja madirisha na milango na kuharibu vitu mbalimbali vilivyokuwepo katika nyumba hiyo wakiwa wanataka……


Baada ya hapo raia wema walitoa taarifa kituo cha polisi ambapo askari waliokuwa doria walifika haraka eneo la tukio na kukuta tayari wahalifu hao wamekimbia. 


Msako mkali wa kuwatafuta wale wote wanaotuhumiwa kuhusika kwa namna moja au nyingine katika uhalifu huo bado unaendelea. 


Pia msako na ufuatiliaji wa vijana wanaotuhumiwa kufanya uhalifu mtaani hapo pamoja na wazazi wao bado unaendelea. 


Pia hakuna mtu yeyote aliyejeruhiwa au kupoteza maisha katika tukio hilo, aidha thamani halisi ya vitu vyote vilivyoharibiwa katika uhalifu huo bado haujafahamika.


Kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza Naibu Kamishina wa polisi Ahmed Msangi anatoa onyo kwa watu wote wenye tabia za kujichukulia sheria mkononi kuacha mara moja kwani ni kosa kisheria na wale wote waliohusika endapo watabainika hatua kali za kisheria zitachuliwa dhidi yao. 


Sambamba na hilo pia anawataka wananchi watambue kwamba dhamana ni haki ya mtuhumiwa endapo tu kama kesi anayohumiwa nayo inadhaminika hivyo wananchi waache tabia ya kujichukulia sheria mkoni pindi watuhumiwa wanapofikishwa mahakamani na kuachiliwa kwa dhamana kwani ni hitaji la kisheria wakati shauri linaendelea mahakamani. 


Aidha anawaomba wananchi kuendelea kutoa taarifa mapema za wahalifu ili waweze kukamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.


IMETOLEWA NA:
DCP: AHMED MSANGI
KAMANDA WA POLISI (M) MWANZA.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527