UINGEREZA YAENDELEZA KICHAPO..... YAIBABUA SWEDEN 2 - 0


Kikosi cha England.
Timu ya taifa ya England imefanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali ya Kombe la Dunia kwa mara ya tatu katika historia ya fainali hizo, baada ya kuifunga timu ya taifa ya Sweden kwa mabao 2-0 kwenye mchezo wa robo fainali uliomalizika jioni hii.

Katika mchezo huo mabao ya England yamefungwa na mlinzi wa Leicester City Harry Maguire dakika ya 30, ambalo pia lilikuwa bao lake la kwanza kwa timu ya taifa ya England pamoja na Dele Alli ambaye alifunga dakika ya 58.

England sasa imefuzu hatua ya nusu fainali kwa mara ya tatu ikianza mwaka 1966 ambapo ilikuwa mwenyeji wa Fainali na iliibuka bingwa kwa mara ya kwanza. Pia ilifika nusu fainali katika fainali zilizofanyika nchini Italia mwaka 1990.

Kwa upande wake Dele Alli ameweka rekodi ya kuwa mchezaji wa pili mwenye umri mdogo kuifungia England bao akiwa na miaka 22 na siku 87. Ametanguliwa na Michael Owen aliyefunga mwaka 1998 dhidi ya Romani akiwa na miaka 18 na siku 190.

England sasa inasubiri mechi ya usiku kati ya Croatia dhidi ya wenyeji Urusi ambayo itaamua ni timu gani itacheza nusu fainali. Timu zingine zilizofuzu hatua ya nusu fainali ni Ufaransa waliowafunga Uruguay 2-0 na Ubelgiji waliowatoa Brazil kwa mabao 2-1.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527