Friday, July 13, 2018

HALMASHAURI YA BUHIGWE,OFISI YA MBUNGE ZAENDESHA MAFUNZO KWA WAJASIRIAMALI

  Malunde       Friday, July 13, 2018
Halmashauri ya wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma, kwa kushirikiana na ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Buhigwe Albert Obama imeendesha mafunzo kwa wajasiriamali wadogo wadogo wilayani humo kwa  lengo la kuongeza ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri na kuongeza uelewa kwa wajasiriamali.


Akizungumza wakati wa mafunzo hayo jana wilayani Buhigwe, mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Anosta Nyamoga alisema semina hiyo inalenga kuongeza mapato kwa halmashauri kwa kuwa wajasiriamali wakiongeza kipato hata pato la halmashauri linaongezeka kupitia ukusanyaji wa kodi na kuboresha maisha ya wananchi na sehemu ya utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi kuwawezesha na kuwapa mafunzo wajasiriamali wadogo wadogo.

Alisema asilimia kubwa ya mapato ya wilaya ya Buhigwe yanategemea ukusanyaji wa ushuru wa mazao na kodi kutoka kwa wajasiriamali wadogo hivyo kupitia semina hiyo wajasiriamali  wataweza kutengeneza bidhaa zenye ubora na kutumia masoko ya ya nje kuuza bidhaa zao na kuongeza kipato chao.

Alisema kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2016/2017 walikusanya shilingi milioni 450 na kwa mwaka wa fedha 2017/2018 wamekusanya milioni 550 na malengo ya wilaya hiyo ni kufikia kukusanya kiasi cha shilingi bilioni moja ifikapo 2020 kutokana na miundombinu ya biashara kuboresha na kukamilika kwa soko la ujirani mwema litakalojengwa Manyovu, ambapo wanatarajia kukusanya zaidi ya milioni 100 kupitia soko hilo.

"Wilaya ya Buhigwe tumejipanga ipasavyo kuhakikisha wananchi wetu wanatoka kwenye maisha waliyokuwa nayo ya kufanya biashara kwa ajili ya kupata chakula kwa sasa tunataka waanze kufanya biashara kwa malengo zaidi kwa kuwa fursa ni nyingi na wananchi walikuwa hawazitumii tunaamini kupitia semina hii uchumi utaongezeka na manufaa watayaona", alisema mkurugenzi huyo.

Awali akifungua mafunzo hayo Mkuu wa wilaya ya Buhigwe Brigedia Jenerali Marco Gaguti aliwataka wafanyabiashara hao kutumia mafunzo hayo kuongeza uelewa na uzalishaji kwa kuwa serikali imejipanga kumuwezesha kila mwananchi na nchi kwa ujumla kufika uchumi wa kati.

Aidha aliwataka kutumia fursa ya somo la nje kwa kuwa vizuizi vilivyokuwepo vimeondolewa na serikali ina mkakati wa kuifungua wilaya hiyo na mikoa mingine kwa kuboresha miundombinu ya usafirishaji hivyo watumie fursa hiyo kuzalisha mazao ya kutosha na kuongeza thamani mazao yao ili uchumi wao uendelee zaidi.

"Wilaya yetu tumependelewa zaidi, tuko mpakani mwa nchi tatu Burundi, Congo na Rwanda ninaamini wananchi wakitumia fursa hii vizuri nina hakika uchumi wa wananchi wetu utaongezeka na tutaifungua wilaya ya Buhigwe ambayo ilikuwa nyuma tumeanza kwa semina hii ninaamini wafanyabiashara hawatakuwa vile walivyowatainuka zaidi", alisema Brigedia Gaguti.

Mbunge wa Jimbo la Buhigwe Albert Obama alisema changamoto aliyokuwa akiipata kwa wawekezaji waliokuwa wakitaka kwenda kuwekeza katika wilaya hiyo ni pamoja na kukosekana kwa umeme kwa sasa umeme umefika na masoko ya ujirani mwema yanajengwa amewaomba wawekezaji kwenda kuanzisha viwanda vya juisi na usindikaji kwa kuwa wilaya hiyo ni wilaya inayozalisha matunda mengi, kahawa pamoja na ndizi.

Obama alisema mafunzo hayo yataleta msukumo mpya kwa wananchi wa Buhigwe kutumia fursa kwa kujua namna ya kuongeza ubora na thamani ya mazao wanayozalisha na kuinua uchumi wao kwa namna bora ya uwekezaji na kutumia masoko ya ujirani mwema kama chachu ya maendeleo kwao.


Kwa upande wake mfanyabiashara Leonard Kataga alisema biashara ya kahawa ndiyo biashara wanayoitegemea hivyo zao hilo likipatiwa soko na kuongezewa uthamani wana hakika zao hilo linaweza kuinua uchumi wao haraka na kuomba serikali kuwasaidia katika zao hilo iliwaweze kuzalisha kwa wingi.

Alisema wananchi wamefurahia  hatua ya serikali kuwapatia mafunzo na kuongeza kuwa mafunzo hayo ni chachu kwao kuwafanya waendelee mbele na kuweza kuongeza thamani katika uzalishaji na kutumia fursa zilizopo kuongeza kipato chao.

Na Rhoda Ezekiel - Malunde1 blog

Usikubali kupitwa na habari..Pakua App ya Malunde1 blog HAPA Ili tuwe tunakutumia habari moja kwa moja Kwenye Simu yako
Loading...
logoblog

Kama Una Habari,Picha,Video,Tangazo n.k Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 757 478 553 ,0625 918 527

Malunde 1 blog Ipo PlayStore....Pakua App yetu mpya HAPA Upate Habari Mpya Moja Kwa Moja Kwenye Simu yako..Utasoma habari hata kama hauna MB..Bofya Hapa
https://play.google.com/store/apps/details?id=com.malunde.blog
Previous
« Prev Post