TFDA YAENDESHA KIKAO KAZI KWA WAHARIRI NA WAANDISHI WA HABARI MIKOA YA SHINYANGA NA MWANZA


Mamlaka ya Chakula na Dawa nchini TFDA limeendesha kikao kazi cha wahariri na waandishi wa habari mikoa ya Shinyanga na Mwanza kwa ajili ya kuwashirikisha na kuhamasisha kazi na majukumu ya TFDA na kujadiliana kwa pamoja namna ya kupambana katika kuhakikisha kuwa soko la Tanzania lina bidhaa bora,salama na fanisi ili kumlinda mlaji. 

Kikao kazi hicho kimefanyika leo Jumatatu Mei 21,2018 katika ukumbi wa mikutano wa TFDA Kanda ya ziwa uliopo Buzuruga jijini Mwanza ambapo mgeni rasmi alikuwa mkuu wa mkoa wa Mwanza,mheshimiwa John Mongella. 

Kaimu Mkurugenzi Mkuu TFDA, Bi.Agnes Kijo alisema kikao hicho kinahusu uhamasishaji wa sheria ya chakula, dawa na vipodozi.

Bi. Kijo alisema TFDA itaendelea kufuatilia, kuondoa na kuteketeza bidhaa ambazo hazikidhi vigenzo vya ubora, usalama na ufanisi ili kuepusha bidhaa husika kutumika ambapo amewahimiza washiriki kufikisha elimu watakayoipata kwa wananchi.

Alisema TFDA imeendelea kutoa elimu kwa wadau mbalimbali kuhusu usalama, ubora, ufanisi wa vyakula, dawa, vipodozi, vifaa tiba pamoja na vitendanishi ili kusaidia kuondokana na matumizi ya dawa na vyakula vyenye madhara.

Aliongeza kuwa hatua hiyo imesaidia TFDA kutekeleza vyema majukumu yake ambapo kwa mwaka 2015/17 usajili wa bidhaa umeongezeka kutoka bidhaa 7,010 hadi kufikia 9,180 hii ikiwa ni ishara njema ya kuwepo ongezeko la uelewa wa matakwa ya sheria miongoni mwa wafanyabiashara.

Akifungua kikao hicho,Mongella alivipongeza vyombo vya habari,wahariri na waandishi wa habari ambao wamekuwa wakitoa taarifa mbalimbali kuhusu umuhimu wa kudhibiti bidhaa unaofanywa na na TFDA na hivyo kuongeza uelewa kwa jamii.

Baadhi ya wanahabari walioshiriki kikao hicho wamesema bado kuna changamoto ya bidhaa zenye viambata sumu kuingia sokoni hivyo watatumia vyema vyombo vyao vya habari kufikisha elimu kwa jamii ili kujiepusha na matumizi ya bidhaa hizo.
Mkuu wa Mkoa Mwanza John Mongella akifungua semina hiyo.Picha kwa hisani ya BMG Habari
Kaimu Mkurugenzi Mkuu TFDA, Bi.Agnes Kijo akizungumza kwenye semina hiyo Mgeni rasmi, viongozi wa TFDA pamoja na washiriki wakiwa kwenye picha ya pamoja. Mgeni rasmi akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi mbalimbali wa TFDA.
Dawa bandia na duni ni hatari kwa mtumiaji. Wanahabari na wahariri wametakiwa kutumia elimu waliyoipata kuelimisha wananchi kuhusu matumizi yasiyo sahihi ya bidhaa zenye viambata sumu. Kaimu Mkurugenzi Mkuu TFDA, Bi. Agnes Kijo (kushoto) pamoja na Naibu Mkurugenzi Idara ya Habari Maelezo, Bi.Zamaradi Kawawa (kulia). Baadhi ya washiriki kutoka mkoani Shinyanga. Mshiriki kutoka Mwanza. Wanahabari wamehimizwa kushirikiana na TFDA kutoa taarifa za uwepo wa bidhaa zenye viambata sumu. Baadhi ya washiriki wa semina hiyo pamoja na Afisa Habari TFDA Kanda ya Ziwa (katika), Martin Malima. Washiriki wa semina. Semina hii imefanyika ukumbi wa TFDA Buzuruga Jijini Mwanza. Tazama video hapa





Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527