MHADHIRI WA CHUO KIKUU UDOM AUAWA KWA KUCHOMWA KISU


MHADHIRI wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Rose Mndenye (31), anadaiwa kuuawa na mume wake kwa kile kinachodaiwa wivu wa mapenzi.

 Akizungumza na waandishi wa habari, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Dk Caroline Damiani alisema walimpokea mhadhiri huyo jana saa 5.30 usiku.

Dk Damian alisema Mdenye alifikishwa hospitalini hapo akiwa tayari ameshakufa huku akiwa na majeraha makubwa katika mwili wake.

 Alisema mwili huo ulifikishwa hospitalini hapo ukitokea katika eneo la Swaswa umbali wa kilometa 15 kutoka katikati ya Jiji la Dodoma.

 “Tulimpokea jana usiku saa 5.30 usiku, alikuwa tayari ameshafariki, alikuwa na majeraha sehemu za mwili wake,” alisema Dk Damian. 

Naye Ofisa Uhusiano wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Beatrice Mtenga alisema walipata taarifa za mhadhiri huyo kuchomwa kisu na mume wake jana usiku.

“Tulipata taarifa jana na sababu ya kifo ni kuchomwa kisu na mumewe wake, sababu wivu wa mapenzi,” alidai ofisa uhusiano huyo. Mtenga alipohojiwa kama anamjua mumewe, alisema hawamjui, lakini wanaendelea kutafuta habari zake na watatoa taarifa baadaye.

Alipotafutwa Kamanda wa Polisi wa Jiji la Dodoma, Gilles Muroto alithibitisha kutokea kwa tukio hilo, huku akidai kwamba Jeshi la Polisi linaendelea kufanya uchunguzi kuhusu chanzo cha kifo hicho. 

Taarifa kutoka nyumbani kwao Swaswa zilidai Mdenye aliuawa na mumewe John Mwaisango na alimuua saa 2.27 usiku akiwa jikoni, Mwaisango amekimbia, anatafutwa hajapatikana.
Theme images by rion819. Powered by Blogger.