ASKOFU WA KANISA LA KKKT APIGWA MAWE


Askofu Ambele Mwaipopo.

ASKOFU wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) Dayosisi ya Ziwa Tanganyika mkoani Rukwa jana alifukuzwa kwa mawe baada ya baadhi ya waumini kumzuia kuingia usharikani wakidai hawataki kumuona akiwepo eneo la kanisa.

Tukio hilo ambalo lilishuhudiwa na mwandishi wa habari lilitokea saa 2:00 asubuhi katika Usharika wa Sumbawanga Mjini, muda mfupi baada ya Askofu Ambele Mwaipopo kufika.

Kumezuka mgogoro baina ya waumini na uongozi wa dayosisi kufuatia mchungaji kiongozi kipenzi cha washarika kuhamishwa.

Askofu Mwaipopo alikuwa ameongozana na Mkuu wa Jimbo la KKKT Katavi, mchungaji Daud Moshi, mchungaji kiongozi wa usharika Zebedayo Mbilinyi na wajumbe wa kamati ya uongozi ya dayosisi hiyo.

Askofu huyo pamoja na kufika kwa ajili ya kushiriki ibada ya jana, pia ilikuwa amtambulishe rasmi Mchungaji Mbilinyi katika kituo chake kipya cha kazi kumrithi Calvin Kessy aliyepewa barua ya uhamisho.

Kwa muda wa siku tatu mfululizo mpaka jana askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) cha Jeshi la Polisi walikuwa wakishinda katika eneo la kanisa hilo, ili kulinda usalama kutokana na hofu ya kuibuka ghasia.

Baada ya Askofu Mbilinyi kufika kanisani hapo jana akiwa ameongozana na ujumbe huo na akidhani angekwenda moja kwa moja ndani ya kanisa, waumini walianza kuimba nyimbo za kumkataa na baada ya muda walianza kumrushia mawe.

Kitendo cha kupigwa mawe kilisababisha askofu huyo na ujumbe wake kila mmoja kukimbilia ndani ya gari lake na kuondoka, wakiwaacha FFU wakijaribu kutuliza waumini hao.

Baada ya FFU kufanikiwa kutuliza vurugu hizo, baadhi ya waumini waliingia kanisani na Mwinjilisti Aniseth Msangawale aliyeongoza ibada mpaka mwisho kabla ya kutawanyika kurejea makwao.

Baadhi ya waumini hawataki kumuona askofu huyo akisali katika usharika mkuu huo kwa madai ya kumhamisha kinyume cha utaratibu mchungaji wao.

UBABE NA HILAWaumini hao wamekuwa wakipinga kuhamishwa kwa Mchungaji Kessy wakidai uhamisho wake umefanyika kwa ubabe na hila, na kwamba amenyimwa hata fursa ya kuwaaga licha ya kuwaongoza kwa muda mrefu.

Aidha, waumini hao wanadai kuwa uhamisho wa mchungaji Kessy umetokana na maslahi binafsi ambapo baadhi ya wajumbe wa kamati ya dayosisi hawataki kumuona mchungaji huyo kwa kuwa amekuwa akifuatilia na kudhibiti mapato ya Usharika wa Sumbawanga Mjini walio ndani na nje kwa ajili ya ujenzi wa Kanisa Kuu la Dayosisi ya Tanganyika.

Akizungumza na gazeti hili, Katibu wa Dayosisi ya Tanganyika, Fredrick Nyamoga alisema waumini wanaogomea uhamisho wa Mchungaji Kessy wanapaswa kutii mamlaka kwani ni wa kawaida.

Naye mmoja wa waumini hao, Baraka Lyimo alisema hawakatai kuhamishwa kwa Mchungaji Kessy, lakini wasichofurahia ni mchungaji huyo kupewa uhamisho baada ya mvutano kuibuka baina yake na Askofu Mwaipopo.

Zelubaberi Luvanda, muumini wa usharika huo alisema Mchungaji Kessy alikuwa akijitahidi kuhamasisha waumini kuchangia michango kwa ajili ya ujenzi wa kanisa hilo sambamba na kudhibiti matumizi hali iliyosababisha apewe uhamisho.

Chanzo- Nipashe

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post