DC NDAGALA AKABIDHI MASHINE YA KUCHAKATA MIHOGO KIKUNDI CHA MWENDO WA SAA KAKONKO

Wakulima wilayani Kakonko Mkoani Kigoma wametakiwa kulima kilimo cha biashara na kuachana na kilimo cha kujikimu wenyewe ili kuondokana na umaskini.

Wito huo ulitolewa jana katika kijiji cha Kiga wilayani Kakonko na Afisa Kilimo wa mkoa wa Kigoma, Joseph Lubuye wakati wa ugawaji wa mashine ya kuchakata mihogo kwa kikundi cha Mwendo wa saa, iliyotolewa na shirika la BTC kupitia mradi wa kilimo wa ENABEL unaotekelezwa na serikali ya Ubergiji na Tanzania, kuendeleza kilimo cha muhogo na maharage kwa kuwakopesha wakulima mashine na kuwapatia mafunzo ya namna ya kulima kitaalamu.

Lubuye alisema wakulima wanatakiwa kubadilika na kuanza kilimo cha biashara na mashine hiyo waliyoipata itumike kuchakata mazao mengi ya mihogo waliyo ima kutokana na maombi na andiko lao la kuomba mashine ya kuchakata mihogo na kufanya uzalishaji wa zao hilo kwa wingi ili wakulima wengine wajifunze kupitia kikundi hicho kutokana na uzalishaji watakaoufanya kupitia mafunzo ya kilimo cha biashara waliyoyapata kuongeza uzalishaji na ubora.

Akikabidhi mashine hiyo yenye thamani ya shilingi milioni mbili na yenye uwezo wa kuzalisha kilo 700 kwa saa moja na hufanya kazi kwa muda wa masaa nane, Mkuu wa wilaya ya Kakonko kanali Hosea Ndagala aliwaasa wakulima kuacha kuuza mazao ambayo hayajaongezwa thamani na kutumia fursa hiyo ya mashine waliyopatiwa kuinua uchumi wao na kulima kitaalamu ili kuongeza uzalishaji.

Aidha mkuu huyo alisema serikali ya awamu ya tano ina lengo la kuongeza viwanda na kikundi cha Mwendo wa saa wameonesha nia ya uanzishwaji wa viwanda kwa kuonesha mfano na kuwataka wananchi wengine kujifunza kupitia vikundi vilivyofanikiwa na waache maneno ya kuongea na sasa wananchi waanze kuanzisha viwanda kwa vitendo.

"Niwapongeze wanakikundi wa Mwendo wa saa kwa juhudi mnazozifanya kuhakikisha mnaondokana na umaskini kwa kilimo cha muhogo, niwaombe wakulima mjitahidi kulima kwa kufuata maelekezo ya wataalamu ili kilimo mtakacholima kiwe chenye tija kitakachowasaidia kutoka mahali fulani na kuinua uchumi wenu, serikali imewapatia mashine hii muitumie kuzalisha zaidi masoko yapo na wafadhili wa mradi huu wameahidi kuwatafutia masoko niwaombe muitumie fursa hii na kuwafundisha wengine waige kwenu", alisema Kanali Ndagala. 


Aidha aliwaomba wananchi kubadilika na  kulima kibiashara na kuacha kulima kilimo cha kujikimu ili kuweza kuondokana na umaskini kulima kilimo cha kisasa na kuacha kulima kilimo kisicho na tija na kutumia mbegu bora kusikiliza wanayowashauriwa na wataalamu wa kilimo.

Kwa upande wake Katibu wa kikundi cha Mwendo wa saa Daudi Bukuku alisema kikundi kina jumla ya wanachama 25 kati yao wanawake ni 12 na wanaume 13 na  kikundi kilianza kwa kununua na kukopeshana hisa huendeshwa kwa kuzingatia sheria, kikundi kina mifuko mitatu ya kujiingizia kipato, mfuko wa hisa ambao una kiasi cha shilingi milioni 13, mfuko wa elimu na afya wenye shilingi milioni mbili na mfuko wa faini na zawadi laki tatu.

Alisema kikundi kinaendesha na shughuli za kilimo kwa ajili ya kukuza kipato ambapo kina hekari tano za migomba ya kisasa, hekari 16 za mihogo na hekari mbili za maharage katika vijiji vya kitangaza na mkombozi.

Hata hivyo alisema matarajio ya kikundi ni ifikapo 2021 ni kuwa na hekari 30 za mihogo na hekari moja moja kwa kila mwanakikundi na kikundi kuhama kutoka vikoba na kuwa Sacoss , huku akibainisha kuwa changamoto ni ukosefu wa mashamba ya kutosha na masoko pamoja na mafunzo ya mara kwa mara ya kuwaelimisha namna bora ya kilimo.
Na Rhoda Ezekiel - Malunde1 blog 
Mkuu wa wilaya ya Kakonko kanali Hosea Ndagala akikabidhi mashine ya kuchakata mazao kwa kikundi cha Mwendo wa saa




Shamba la mihogo


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527