DC JENERALI GAGUTI AWAPONGEZA WANANCHI KUJITOLEA KUJENGA SHULE KUNUSURU WANAFUNZI 600

Zaidi ya wanafunzi 600 wa darasa la tatu katika shule ya Msingi Kumkambati kata ya Nyamidaho wilayani Kasulu mkoani Kigoma, wanalazimika kusoma katika chumba kimoja kutokana na uhaba wa madarasa na wingi wa wanafunzi hali iliyowalazimu wazazi kuanzisha ujenzi wa shule nyingine katika vijiji jirani vya Kumtundu na Mkuyuni.

Hayo yalibainika jana wakati wa ziara ya mkuu wa wilaya ya Kasulu Brigedia Jenerali Marco Gaguti wakati akitembelea miradi ya wilaya hiyo iliyoanzishwa na wananchi na inayofadhiliwa na serikali ambapo alifika katika Shule ya msingi Kumtundu iliyoanza kujengwa kwa juhudi za wananchi wa Kijiji hicho ili kupunguza wingi wa wanafunzi katika shule iliyopo katika kijiji jirani cha Mvungwe.

Akitoa taarifa ya shule hiyo mkuu wa Shule ya Msingi Kumkumbati Faresi Lugati alisema shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 2024 na jumla ya walimu 14 na darasa la tatu ndilo lina wanafunzi 600, ambapo wanalazimika kuwagawa awamu mbili ya asubuhi na mchana ili waweze kuwafundisha na kumpunguzia mzigo mwalimu anayefundisha darasa hilo.

Alisema shule hiyo inahudumia wanafunzi wa vijiji viwili na wameanza kutatua tatizo la mlundikano wa wanafunzi kwa kujenga vyumba viwili vya madarasa, na wananchi wa kijiji cha Kumtundu wameanza ujenzi wa shule mpya itakayo saidia kupunguza wanafunzi waliopo katika shule hiyo kuhamia katika shule jirani inayojengwa.

Akisoma taarifa ya ujenzi wa Shule hiyo Katibu wa kamati ya ujenzi wa shule ya msingi Kumtundu Raphael Zacharia alisema wameanza ujenzi wa madarasa manne na ofisi moja na ujenzi wa msingi na ukuta pamoja na upauaji umekamilika na jumla ya gharama ni shilingi milioni 14 na milioni 11 zimechangwa na wananchi na Waziri wa Elimu alichangia shilingi milioni tatu. 

Alisema changamoto ni upungufu wa vifaa vya ujenzi uhaba wa kifungu cha fedha kuwalipa mafundi na kuomba serikali kuunga mkono kuchangia vifaa vya ujenzi ilikukamilisha ujenzi pamoja na upatikanaji huduma za maji.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Kasulu Brigedia Jenerali Marco Gaguti aliwapongeza wananchi kwa hatua hiyo waliyoichukua ya kuona upungufu wa vyumba vya madarasa na kuona wanafunzi wanavyoteseka na kuamua kutafuta shule nyingine ili waweze kutatua tatizo la wanafunzi kutembea umbali mrefu kufuata huduma ya shule.

Alisema ataendelea kuhimiza fedha inayotakiwa kutolewa kwa ajili ya kumalizia shule hiyo ianze, na kuahidi kuchangia shilingi milioni mbili kutoka katika mfuko wa mkuu wa wilaya ili ziweze kuiongezea kwenye vifaa ambavyo bado havijanunuluwa.

Aidha mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Kasulu Godfrey Kasekenya alisema  wamejipanga kuhakikisha shule hiyo inakamilika Januari 2019 wanafunzi wanaanza kusoma na wao kama halmashauri wamejiandaa kukamilisha matundu 10 ya vyoo kupitia mfuko wa EPFORR kiasi cha shilingi milioni nane zimetengwa kwa ajili ya shughuli hiyo.


Akiwa katika ziara yake,Brigedia Jenerali Gaguti alitembelea vituo viwili vya afya vya Nyamidaho na Nyakitonto vituo vya Afya vinavyo jengwa kwa fedha za serikali kuu kwa kutuma utaratibu wa Force Account ambapo aliwapongeza viongozi wa vijiji na wananchi kwa kujitolea kukamilisha ujenzi huo kwa gharama nafuu na kazi inaendelea vizuri na kuwataka wananchi wote kuendelea kushirikiana na serikali katika shughuli za maendeleo.
Na Rhoda Ezekiel - Malunde1 blog













Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527