Friday, April 6, 2018

Picha : WANAODAIWA VINARA WA MAUAJI YA WANAWAKE SHINYANGA WANASWA ...WAKUTWA NA CHUPI, KARATASI YA MAJINA 'KILL THEM ALL'

  Malunde       Friday, April 6, 2018
Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga linawashikilia watu watano akiwemo mganga wa kienyeji kwa tuhuma ya kujihusisha na mauaji ya kukata mapanga wanawake katika kata ya Salawe Shinyanga vijijini kutokana na imani za kishirikina.
 
Hayo yamebainishwa leo Aprili 6,2018 na Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Kamishina msaidizi wa Polisi (ACP) Simoni Haule wakati akizungumza na wananchi wa kata hiyo kwenye mikutano ya hadhara miwili iliyofanyika katika kijiji cha Mwenge na Songambele. 

Amewataja watuhumiwa waliokamatwa kuhusika na mauaji hayo kuwa ni Stephano Maduka (20), Nihinga Lendele (57) Reuben Mafura (30) Amosi Itawa (21) pamoja na mganga wa kienyeji Itawa Ming’hwa (47) ambapo wote wapo chini ya ulinzi wa jeshi hilo na upelelezi ukikamilika watafikishwa mahakamani kujibu mashtaka yanayowakabili. 

Amesema walipofanya upekuzi nyumbani kwa mganga huyo wa kienyeji alikutwa akiwa na mkia wa mnyama adhaniwaye kuwa ni nyati, ngozi ya kenge, kipande cha ngozi ya Fisi, Pembe nne za wanyama mbalimbali,shuka tano nyeusi za kaniki, karatasi nakala tatu zenye maandishi “KILL THEM ALL” kifaranga cha kuku kinachotumika kupigia ramli chonganishi. 

Ametaja vitu vingine kuwa ni chupi moja ya kike, mafungu mbalimbali ya mchanga, mawe yadhaniwayo kuwa ni madini ambayo yanatumika kupigia ramli chonganishi, pamoja na karatasi ikiwa na majina ya wanawake tisa ambao wamepangwa kuuawa ili kukamilisha ushirikina huo. 

“Baada ya kuwahoji watuhumiwa hao baadhi yao wamekiri kuhusika na mauaji haya kwa madai waliagizwa na waganga wa kienyeji kwa kutoa kafara za wanawake tisa kama ndagu ili dawa zipate kufanya kazi na kupata utajiri,”,amesema Haule 

Pia Kamanda  Haule amewataja wanawake watatu ambao wameshauawa kwenye imani hizo za kishirikina kuwa ni Mwalu Misri (24) Salome Paschal (24) Kabunga Linonelwa(10) ambao waliuawa kwa nyakati tofauti kuanzia kipindi cha Januari hadi Machi mwaka huu kwa kuviziwa kwenye vichaka na kisha kuuawa. 

Katika hatua nyingine Kamanda ametoa wito kwa wananchi hasa vijana kuacha kutafuta mali kwa njia za ushirikina bali wajiunge kwenye vikundi vya ujasiriamali ili waweze kukopesheka na kufanya kazi halali ambazo zitawaingizia kipato na kuinuka kiuchumi. 

Nao baadhi ya wanawake waliohushuria kwenye mikutano hiyo ya hadhara Neema Paulo na Happynes Jeremia wameiomba serikali kukomesha kabisa matukio hayo ya mauaji dhidi yao ambayo yamekuwa yakiwafanya kushindwa kwenda kufanya shughuli za kiuchumi ikiwamo mashambani kwa kuhofia kuuawa. 

TAZAMA MATUKIO KATIKA PICHA HAPA CHINI
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Kamishina msaidizi wa Polisi (ACP) Simon Haule akiwa na wananchi akiongozana nao kwenda kuona vichaka ambavyo vilitumika kwa mauaji ya wanawake watatu kwa imani za kishirikina katika kata ya Salawe.Picha zote na Marco Maduhu- Malaunde1 blog & Shinyanga News Blog
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Kamishina msaidizi wa Polisi (ACP) Simon Haule akiwa na wananchi akiongozana nao kwenda kuona vichaka ambavyo vilitumika kwa mauaji ya wanawake watatu kwa imani za kishirikina.
Wananchi wa kitongoji cha Ituli Kijiji cha Songambele Kata ya Salawe wakiwa na Jeshi la Polisi kwenye vichaka ambavyo vilitumika kutekelezwa kwa mauaji ya wanawake watatu wasio na hatia sababu ya imani potofu ya kishirikina.
Diwani wa Kata ya Mwenge Edward Maganga akionyesha sehemu ambayo mtoto wa kike Kabunga Linonelwa alipouawa na watu hao.
Wananchi wakiwa eneo la tukio yalipotekelezwa mauaji.
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Kamishina msaidizi wa Polisi (ACP) Simon Haule akiwa na wananchi wakiangalia maeneo ambayo yalitekelezwa mauaji.
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Kamishina msaidizi wa Polisi (ACP) Simon Haule akionyesha baadhi ya dhana ambazo zilikutwa kwa mganga wa kienyeji ambaye alikuwa akivitumia kupiga ramli chonganishi na kusababisha mauaji ya wanawake hao watatu.
Dhana ambazo zilikuwa zikitumiwa na mganga huyo wa kienyeji kupigia ramli chonganishi na kusababisha mauaji ya watu wasio na hatia.
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Kamishina msaidizi wa Polisi (ACP) Simon Haule akionyesha mkia wa nyati ambao umekatwa kwa mganga huyo wa kienyeji.
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Kamishina msaidizi wa Polisi (ACP) Simon Haule akiwa na viongozi wa serikali ya kijiji cha Mwenge wakipiga picha ya pamoja kuashiria sasa amani ina tawala kwenye kijiji hicho.
Jeshi la Jadi Sungusungu likiwa kwenye mkutano wa hadhara wa Jeshi la Polisi na kuombwa wafanye kazi zao kwa weledi kwa kushirikiana na jeshi hilo kutokomeza uharifu ndani ya jamii.

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Kamishina msaidizi wa Polisi (ACP) Simon Haule akiwaapisha wananchi wa kijiji cha Mwenge kuachana na imani za kishirikina ambazo zimekuwa zikisababisha mauaji ya watu wasio na hatia.
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Kamishina msaidizi wa Polisi (ACP) Simoni Haule akizungumza na wananchi wa kijiji na kata ya Mwenge tarafa ya Nindo kwenye mkutano wa hadhara kuacha kuendekeza imani za kishirikina ambazo zimekuwa zikisababisha mauaji ya watu wasio na hatia.
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP) Simoni Haule akitaja majina ya watu watano waliokamatwa wakituhumiwa kuhusika na mauaji ya wanawake kwa kuwakata mapanga sababu ya imani za Kishirikina kuwa ni Stephano Maduka (20), Nihinga Lendele (57) Reuben Mafura (30) Amosi Itawa (21) pamoja na mganga wa kienyeji Itawa Ming’hwa (47) huku akionyesha Karatasi ambayo ilikutwa kwa mganga huyo wa kienyeji ikiwa na majina Tisa ya wanawake ambao wanatakiwa kuuawa ikiwa na kichwa cha habari KILL THEM ALL.
Wanawake wa Kijiji cha Mwenge wakiwa kwenye mkutano wa hadhara wa Jeshi la Polisi juu ya kurejesha amani kwenye kijiji hicho.
Wanawake wa kijiji cha Mwenge wakiwa kwenye mkutano wa hadhara wa Jeshi la Polisi juu ya kurejesha amani kwenye kijiji hicho.
Wanaume wa Kijiji cha Mwenge wakiwa kwenye mkutano wa hadhara wa Jeshi la Polisi juu ya kurejesha amani kwenye kijiji hicho.
Wanawake wa Kijiji cha Mwenge wakiwa kwenye mkutano wa hadhara wa Jeshi la Polisi juu ya kurejesha amani kwenye kijiji hicho.
Mmoja wa mwanamke Mariam Sweya ambaye anaomba kusaidiwa na Serikali mara baada ya kutengwa na wanakijiji wenzake kwa tuhuma za kuhusika na imani za kishirikina na kutekelezwa kwa mauaji hayo ya wanawake wenzake na kuahidiwa tatizo lake linashughulikiwa kisheria.
Neema Paulo ni mwanamke anayeishi katika kijiji hicho cha Mwenge akiiomba Serikali kumaliza kabisa matukio hayo ya mauaji dhidi yao ambayo yamekuwa yakiwakwamisha kufanya shughuli zao za kiuchumi ikiwamo kutokwenda shambani.
Mkuu wa upelelezi mkoani Shinyanga Amedius Tesha amewatahadharisha watu ambao wataendelea na mauaji hayo ya watu wasio na hatia kuwa Serikali itawashughulikia pamoja na kuwafunga Jela.
Awali Mwenyekiti wa kijiji cha Songambele Kata Salawe Lazaro Enock akifungua mkutano wa hadhara wa Jeshi la Polisi wenye lengo la kurudisha amani ambayo ilitoweka ndani ya miezi mitatu katika vijiji hivyo viwili kwa wanawake kuuawa bila ya kuwa na hatia sababu ya imani za kishirikina.
Diwani wa Kata ya Salawe Joseph Buyugu akizungumza kwenye mkutano huo wa hadhara ambapo amelipongeza jeshi la polisi mkoani humo kwa kukamata watuhumiwa ambao wanahusika na mauaji ya wanawake ambao hawana hatia.
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Kamishina msaidizi wa Polisi (ACP) Simoni Haule akizungumza na wananchi wa kijiji cha Songambele Kata hiyo ya Salawe na kuwataka kuacha kuendekeza Imani za Kishirikina bali wajitume kufanya kazi kwa bidii na hata wakiugua waende kwenye sehemu za huduma za afya kupatiwa matibabu na siyo kukimbilia kwa waganga wa kienyeji ambao ndio chanzo cha mauaji ya watu hao wasio na hatia kwa kupigiwa ramli chonganishi.

Wananchi wa kijiji cha Songambele kata ya Salawe wakiwa kwenye mkutano wa hadhara wa Jeshi la Polisi wa kurejesha hali ya amani.
Wananchi wa kijiji cha Songambele Kata ya Salawe wakiwa kwenye mkutano wa hadhara wa Jeshi la Polisi wa kurejesha hali ya amani.
Paulo Malemi ni mwananchi wa kijiji cha Songambele Kata ya Salawe akiomba Serikali ya kijiji hicho kufufua Jeshi la Jadi Sungusungu ambalo limekufa na kusababisha matukio ya mauaji dhidi ya wanawake kuendelea kushamili.
Wananchi wa kijiji cha Songambele Kata ya Salawe wakiwa kwenye mkutano wa hadhara wa Jeshi la Polisi wa kurejesha hali ya amani.
Wananchi wa kijiji cha Songambele Kata ya Salawe wakiwa kwenye mkutano wa hadhara wa Jeshi la Polisi wa kurejesha hali ya amani.
Wanawake wa kijiji cha Songambele Kata ya Salawe wakiwa kwenye mkutano wa hadhara wa Jeshi la Polisi wa kurejesha hali ya amani.
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Kamishina msaidizi wa Polisi (ACP) Simoni Haule akiwa na mkuu wa kituo cha Polisi Kata hiyo ya Salawe Mashaka Matongo wa kwanza mkono wa Kushoto na Katikati ni mkuu wa upelelezi mkoani Shinyanga Amedius Tesha wakiangalia eneo la kichaka ambalo lilitekelezwa mauaji ya mwanamke Mwalu Misri.
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga kamishina msaidizi wa Polisi (ACP) Simoni Haule akiangalia maeneo ambayo wanawake hao watatu waliuawa kwenye vichaka katika kitongoji cha Ituli kijiji cha Songambele Kata ya Salawe.
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga kamishina msaidizi wa Polisi (ACP) Simoni Haule akizungumza na wananchi wa Kitongoji cha Ituli Kijiji cha Songambele Kata ya Salawe kwenye maeneo ya vichaka ambapo mauji hayo yametekelezwa na kuwataka kutoa taarifa kwa Jeshi hilo kuwafikichua waharifu wote ikiwa wanafahamika.
Diwani wa Kata ya Mwenge Edward Maganga ameliomba Jeshi hilo pale wananchi wanapotoa taarifa za waharifu kuwepo na usiri ikiwa watuhumiwa wanapoachiwa na kurudi uraiani huanza kuwatishia wale watu ambao waliwataja na hivyo kwa sasa wananchi wamekuwa wagumu kutoa taarifa za uhalifu.
Picha zote na Marco Maduhu- Malaunde1 blog & Shinyanga News Blog
Usikubali kupitwa na habari..Pakua App ya Malunde1 blog HAPA Ili tuwe tunakutumia habari moja kwa moja Kwenye Simu yako
Loading...
logoblog

Kama Una Habari,Picha,Video,Tangazo n.k Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 757 478 553 ,0625 918 527

Malunde 1 blog Ipo PlayStore....Pakua App yetu mpya HAPA Upate Habari Mpya Moja Kwa Moja Kwenye Simu yako..Utasoma habari hata kama hauna MB..Bofya Hapa
https://play.google.com/store/apps/details?id=com.malunde.blog
Previous
« Prev Post