VILIO VYATAWALA IBADA YA MAZISHI YA MMILIKI WA MABASI YA SUPER SAMI

Vilio, simanzi na majonzi vimetawala kwa waombolezaji kutoka jijini Mwanza na maeneo jirani wanaendelea na ibada ya mazishi ya mfanyabiashara Samson Josia yanayofanyika nyumbani kwake mtaa wa majengo mapya wilaya ya Magu mkoani Mwanza.


Mwili wa mfanyabiashara huyo uliokutwa ukiwa umefungwa kwenye viroba ukielea ndani ya Mto Ndabaka mpakani mwa wilaya za Bunda mkoa wa Mara na Busega mkoani Simiyu umewasili asubuhi ya leo Machi 16 ukitokea Hospitali ya Rufaa Mara ulikohifadhiwa kwa ajili ya uchunguzi tangu juzi.


Tangu asubuhi, mamia ya waombolezaji kutoka jijini Mwanza na maeneo jirani wamekuwa wakimiminika nyumbani kwa marehemu wakitumia mabasi ya kampuni aliyokuwa akimiliki.


Mabasi ya kampuni nyingine pia yanatumika kusafirisha waombolezaji kutoka jijini Mwanza bila malipo.


Marehemu Josia aliyezaliwa mwaka 1968 alipotea tangu Februari 27 kabla ya gari lake kukutwa likiwa limeteketezwa kwa moto ndani ya eneo la hifadhi ya Taifa ya Serengeti mkoani Mara Machi 9.


Ibada ya mazishi inaongozwa na Mchungaji Jackson Meza kutoka Kanisa la African Inland Church of Tanzania (AICT) huku kwaya ya kanisa ambayo marehemu alikuwa mfadhili wake ikiimba nyimbo za maombolezo.


Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoa wa Mara, Jaffari Mohamed, watu wanne wanashikiliwa na jeshi hilo kwa mahojiano kuhusiana na kifo hicho kilichoibua hofu na maswali yasiyo na majibu miongoni mwa ndugu, jamaa, marafiki na wakazi wa jiji la Mwanza ambako marehemu alikuwa akiendesha shughuli zake za kibiashara.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527