UTITIRI WA MAKANISA WAMSHTUA RAIS



Wakati Bodi ya Utawala Bora nchini Rwanda (RGB) ikisitisha shughuli za makanisa 714 na msikiti mmoja, kwa kushindwa kufikia vigezo vinavyotakiwa katika kuendesha shughuli zao, Rais Paul Kagame ameelezea kushitushwa na idadi hiyo kubwa ya makanisa nchini mwake.

Rwanda, taifa la Afrika Mashariki lenye wakazi 11,262,564, kwa mujibu wa Sensa ya mwaka 2012, wakazi wake wengi ni Wakristo, hasa Waprotestanti ambao ni asilimia 49.5, Wakatoliki asilimia 43.7 na Waislamu ni asilimia mbili. “Makanisa 700 ndani ya Kigali? Hivi ni visima vinavyowapa watu maji?” alihoji Rais Kagame baada ya kusikia hatua zilizochukuliwa dhidi ya makanisa hayo.

“Sina visima vingi kiasi hiki. Pia tuna idadi kubwa ya viwanda? Lakini makanisa 700, ambayo pia mengine yanafungwa? Hakika inashangaza sana!” Rais Kagame aliyasema hayo hivi karibuni wakati akifunga `semina elekezi’ ya siku nne kwa viongozi wa umma nchini Rwanda. Alisema kwa uelewa na imani yake, Rwanda haijafikia hatua ya kuhitaji idadi kubwa ya makanisa kama inayosikika.

“Kama taratibu zingekuwa zinafuatwa, tusingefikia hatua hii ya kufungia makanisa. Lakini kwa hatua hii, sitashangaa kuona hatua ya Serikali ikipigiwa kelele kuwa ni ukiukwaji wa haki za binadamu. Najua watu wana haki za kuabudu, lakini taratibu lazima zifuatwe,” alisema Rais Kagame. Vigezo vilivyotumika kufungua makanisa na msikiti mmoja, vimetajwa kuwa ni pamoja na kutodhibiti kelele, usafi duni na pia mazingira yasiyo salama kwa waumini wao. “Baadhi ya makanisa yanaendesha ibada katika mazingira hatarishi na yasiyo masafi, kiasi cha kutishia afya na usalama wa watu,” anasema Anastase Shyaka, Mkuu wa RGB inayosimamia taasisi za umma na binafsi nchini Rwanda. “Suala la kelele pia limeripotiwa, hili limekuwa sugu kwa baadhi ya makanisa. Ndiyo maana tumeamua kuchukua hatua. Hatutayaruhusu kufanya kazi hadi hapo yatakaporekebisha dosari,” alisisitiza Shyaka.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527