RAIS MAGUFULI: MSIKUBALI KUWA VILAZA, ATAKAYEWAKWAMISHA NAMBIENI NIMSHUGHULIKIE

Rais Dkt. John Pombe Magufuli amefunguka na kuwaambia viongozi wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kuwa wasikubali kuwa vilaza baada ya kugundua Mamlaka ya Chakula na Dawa, TFDA imekuwa kikwazo kwa Bohari Kuu ya Dawa (MSD).


Rais Magufuli amesema hayo leo Machi 26, 2018 wakati akizundua magari 181 ya Bohari Kuu ya Dawa (MSD) ambayo yanategemewa kuanza kusafirisha dawa mijini na vijinini


Akiwa kwenye uzinduzi huo Rais Magufuli alipokea malalamiko kuwa zipo baadhi ya taasisi za serikali zimekuwa zikichangia kukwamisha ucheleweshwaji wa dawa ambazo zinaletwa na Bohari Kuu ya Dawa (MSD).


"Nimesikia saa zingine kunakuwa na ucheleweshwaji kati ya taasisi fulani fulani ndani ya serikali taasisi ya vyakula TFDA, mnaleta madawa halafu mnashindwa kupata kibali bandarini, madawa yanacheleweshwa inawezekana 'expire date' yake inafika madawa bado yamezuiliwa pale bandarini.


" Mimi atakae zuia madawa haya niambieni ili nijue chombo gani cha serikali, niambieni tu huyo aliyezuia nione ili na mimi nimzuie yeye moja kwa moja,kuna mambo mengine ni rahisi sana wala msilalamike bali mwambie Waziri au Katibu Mkuu" alisema Rais Magufuli


Magufuli aliendelea kuweka wazi kuwa watu ambao wanakwamisha na kuchelewesha dawa kutoka ni watu ambao pia wanatoka katika wizara hiyo hiyo wa Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.


"Hata aliyempa nguvu ya kuzuia dawa wapo chini ya wizara yenu yaani ni nyinyi wenyewe, basi nyinyi vilaza sasa mtu yupo chini yenu, yaani mtu anayezuia yupo kwako anayezuiliwa yupo kwako bado mnakaa mnaimba nini. 


"Mimi nataka haya niyashughulikie unajua mambo mengine mnakwamishana nyinyi wenyewe kama ni TRA mwambie Katibu Mkuu, mwambie Waziri wa Afya, mwambie Waziri wa Fedha tufike mahali tusikwamishane, kwa sababu anaweza akawa amekwamisha madawa yenu lakini madawa ya mtu binafsi anayaruhusu siku hiyo hiyo sasa hili ni lenu wala halihitaji kufika kwangu" alisisitiza Magufuli

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527