POLISI MBARONI KWA KUBAKA MTOTO WA JIRANI YAKE

Askari Polisi namba H.3102 konstebo Bariki Michael (28), wa kituo cha Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi, juzi alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa akikabiliwa na shitaka la kumbaka mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 14 (jina limehifadhiwa).


Michael alifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi, Erasto Phili na kusomewa shitaka linalomkabili na wakili wa serikali, Juma Maige.


Akisoma shitaka hilo, Maige alidai mshitakiwa alitenda kosa hilo Machi 14, mwaka huu saa 4:00 asubuhi eneo la Kilimani mjini Ruangwa.


Wakili huyo alidai kuwa mshitakiwa, akiwa anatambua analofanya ni kosa, alipata mwanya wa kutekeleza tendo hilo nyumbani kwa mtoto huyo, ambaye pia ni jirani yake kufuatia kubaki peke yake, ndipo akaitumia nafasi hiyo kumfuata na kumwingilia kwa nguvu.


Maige alidai kutokana na kitendo hicho, mlalamikaji alipiga kelele za kuomba msaada kutoka kwa majirani ambao walijitokeza na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa huyo na kumpeleka kituo chao cha Polisi cha Ruangwa mjini.


Mshitakiwa alikana kosa na kupelekwa mahabusu baada ya kukosa dhamana na kesi yake imepangwa kutajwa mahakamani hapo April 12.


Wakili wa serikali Maige alisema upelelezi wa shauri hilo umekamilika.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527