POLEPOLE AIBUKIA KWENYE MRADI WA SAMAKI ULIOGEUZWA MALI YA MTENDAJI WA KATA NA VIONGOZI WA KIJIJI KIGOMA



Mradi wa ufugaji wa samaki ulioibuliwa na wananchi na kuendelezwa na serikali kwa lengo la kuzinufaisha kaya maskini katika kijiji cha Biturana Kata ya Biturana Wilayani Kibondo Mkoani Kigoma umegeuzwa kuwa mali ya mtendaji wa kata hiyo na baadhi ya viongozi wa serikali ya kijiji hicho.


Hayo yameibuliwa jana na Katibu wa itikadi na uenezi CCM Taifa Humphrey Polepole Wakati akikagua mradi wa maendeleo wa kuzinufaisha kaya maskini alipotembelea mradi wa Bwawa la samaki na kubaini kuwepo na changamoto.

  Juzi Polepole alifika katika mradi huo na kuweka chakula cha samaki hao bwawani wakashindwa kutokea ikamlazimu kurudi siku ya pili na kubaini kuwa samaki waliomo ni vifaranga na wanufaika wa mradi huo kutumiwa kama vibarua katika mradi huo na mtendaji wa kijiji na baadhi ya viongozi wa kijiji kujinufaisha na mradi huo.

Polepole alisema kwa mujibu wa maelezo ya wanufaika hao walieleza kuwa mradi huo uliibuliwa miezi 10 iliyopita na wao walikuwa wakihudumia samaki hao kwa miezi minne tangu kuanzishwa na kulipwa kiasi cha shilingi 2300/= kwa siku baada ya hapo wamekuwa wakijitolea.

Alisema kwa mujibu wa wataalamu wa mifugo mpaka sasa wananchi wangekuwa wameanza kuuza samaki hao na wangekuwa wamepata zaidi ya shilingi milioni 18 lakini mpaka sasa kwenye hilo bwawa kuna vifaranga vya samaki ambavyo havikui hali iliyoleta sintofahamu kwa wanufaika na wanakijiji na kumtuhumu Mtendaji na baadhi ya viongozi wa serikali ya kijiji kuhujumu mali hiyo kwa kuwa wao ndiyo waangalizi wa mradi huo.

"Wako watu wanafanya mchezo na fedha zinazotolewa na serikali kwa kujinufaisha wao, sisi kama waangalizi wa utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi hatutalifumbia macho jambo hili na kwamba tutahakikisha tunafuatilia",alieleza.

  "Hivi kweli kuna mtu anafurahia kuona samaki miezi tisa hawajakua kweli,  mnatufanya wananchi washindwe kukiamini chama chao tunataka wananchi wanpate haki yao, lengo la serikali ni kuwasaidia wanufaika kuondokana na umaskini na sio miradi hii inayoanzishwa kuwa ya mtu mmoja.. nikuombe Mkuu wa wilaya ukae na watendaji wa halmasharu kuangalia mnalitatuaje hili"alisema Polepole.

Kufuatia hali hiyo,Mkuu wa wilaya ya Kibondo Louis Bura aliagiza mtendaji huyo akamatwe na mkurugenzi wa Halmashauri ya Kibondo kumuondoa Mtendaji wa Kata na Watendaji wengine walio chini yake na kuunda kamati itakayokwenda katika kijiji hicho na kuchunguza mmiliki halali wa mradi huo ni nani na kuhakikisha lengo la serikali linatimia na siyo baadhi ya wa watu kunufaika na fedha zinazotolewa na wananchi.

Aidha Bura alisema hawako tayari kuendelwa kulea mafisadi kwani Serikali ya awamu ya tano ipo kwa ajili ya kuwanufaisha na kuwasaidia wananchi na sio kuwanyanyasa.

Alisema mradi huo ulianzishwa kwa ajili ya kuwasaidia wananchi maskini lakini mpaka sasa ni zaidi ya miezi 10 hakuna kitu ambacho wananchi hao wamekipata na kumuagiza mkurugenzi kuchukua hatua haraka iwezekanavyo.

 Mwananchi wa kijiji cha Biturana Paulo Chubwa alisema mpaka sasa wananchi wananyanyasika wengi wanasema mradi umebinafsishwa na watu wachache na mtendaji anaendesha kijiji  kwa matakwa yake binafsi na amewaandaa wanufaika waseme kuwa mradi huo ni wakwao na wakisema ukweli wanawekwa ndani kweli mradi huo.

Alisema samaki hao hawapewi chakula na vyakula hivyo vimetolewa  kwa walengwa na walengwa wanakuja kama vibarua na mtendaji wa kijiji na Mwenyekiti ndiyo wanojua mradi huo na imefikia hatua wananchi wameamua kuanzisha bwawa jipya baada ya kubaini kuwa bwawa hilo ni mali ya serikali ya kijiji hicho.

Kwa upande wake Balozi Kijiji cha Biturana alisema mtendaji wa kata Aliseni Ruhigwa na mwenyekiti wa kijiji Batromayo Biyagara wamekuwa wakiendesha kijiji hicho kama mali yao na walengwa hao wamekuwa wakijitolea katika mradi huo na kuishia kulipwa kiasi cha shilingi 2300/= kwa siku na wamelipwa kwa kipindi cha miezi minne na baada ya hapo wamekuwa wakijitolea na hakuna wanufaika wanao nufaika na mradi.

Alisema hata mradi ulipokabidhiwa kwa wananchi bado wananchi wa kijiji hicho hawana taarifa yoyote juu ya mradi huo na wanaohusika na mradi huo ni mwenyekiti pamoja na mtendaji na hawatoi ushirikiano kwa wananchi kujua mradi huo.

Alisema afisa mtendaji amekuwa tatizo na amekuwa akikifanya kijiji kama mali yake na kuwafanya wananchi kuwa wanyonge na hahitaji kupokea mradi taarifa aliyopewa ya kuwa mradi umeanza mwezi wa tisa ni uongo na kwamba mradi huo umeanza mwezi wa pili 2017 na hao samaki wakubwa wamekwisha kuchukuliwa na mtendaji na viongozi wengine wa kijiji.

Mratibu wa mfuko wa maendeleo wa kunusuru kaya maskini TASAF wilayani humo John Makunja  alisema wametekeleza miradi ya ajira za muda na ni miradi inayoibuliwa na wananchi na walengwa wanafanya kazi kwa siku 60 na mlengwa atakuwa analipwa kiasi cha shilingi 2300/= kwa siku na baada ya miradi hiyo kukamilika miradi hiyo inakabidhiwa kwa serikali ya kijiji kwa ajili ya kuwanufaisha wananchi wote wakiwemo walengwa na mradi unakuwa chini ya uangalizi wa wananchi.

Alisema katika kijiji hicho walianzisha mradi wa bwawa la samaki ulioibuliwa na wanufaika 175 na kununua vifaranga 6000 na kughalimu kiasi cha shilingi milioni 17 zilizotengwa kwa ajili ya kuzinusuru kaya masikini ambazo zilitumika kuchimba bwawa na upandaji wa miti.

Alisema  baada ya kukamilika mradi huo ulikabidhiwa kwa serikali ya kijiji na anashangazwa na kukuta mradi huo hauna maendeleo kutokana na wao walikuwa wakifika katika eneo hilo walikuwa wanajibu kuwa mradi ni wa wananchi na wanaendelea vizuri.

Na Rhoda Ezekiel-Malunde1 blog

Katibu wa itikadi na uenezi CCM Taifa Humphrey Polepole akiangalia mradi wa ufugaji wa samaki  katika kijiji cha Biturana Kata ya Biturana Wilayani Kibondo Mkoani Kigoma - Picha zote na Rhoda Ezekiel - Malunde1 blog








Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527