MBOWE NA WENZAKE WAGONGA MWAMBA...SASA KULA PASAKA WAKIWA MAHABUSU


Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Wilbard Mashauri amesema baada ya kusikiliza hoja zilizowasilishwa na upande wa Serikali na utetezi katika kesi inayowakabili viongozi wa Chadema, akiwemo mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe washtakiwa hao wafikishwe mahakamani hapo Aprili 3, 2018.


Amesema siku hiyo washtakiwa watasaini bondi ya Sh20 milioni na wakiwa huru ndipo utaratibu wa kukata rufaa wa upande wa mashtaka utafanyika.


Kufuatia uamuzi huo, viongozi hao watakula Sikukuu ya Pasaka wakiwa mahabusu. Sikukuu hiyo inasherehekewa kuanzia kesho hadi Jumatatu.


Awali, Hakimu Mashauri alieleza dhamana kwa washtakiwa hao iko wazi, jambo ambalo lilipingwa na upande wa Serikali.


Washtakiwa hao walitakiwa kila mmoja kuwa na wadhamini wawili ambao watasaini hati ya dhamana ya Sh20 milioni na kuwa na barua kutoka kwa viongozi wao ama wa vijiji au mtaa, ambao watapaswa kuwa na nakala za vitambulisho vyao.


Pia, walitakiwa kuripoti katika Kituo Kikuu cha Polisi, Dar es Salaam.


Hakimu alisema kwa asiyeridhika na uamuzi huo ana haki ya kukata rufaa.


Katika mvutano wa kisheria, mmoja wa mawakili wa viongozi hao, Peter Kibatala alipinga taarifa ya rufaa iliyotolewa na wakili wa Serikali.


Kibatala aliiomba mahakama kutekeleza amri yake ya dhamana kwa kuwasainisha washtakiwa bondi ya Sh20 milioni kila mmoja katika tarehe ambayo inaona inafaa na baada ya hapo ndipo ipokee taarifa ya Serikali ya kukata rufaa.


Wakili wa Serikali, Faraja Nchimbi alidai kuwa hilo ni suala la kisheria kwa kuwa taarifa ya rufaa ikishawasilishwa mahakamani na kupokewa, mahakama husika itakuwa imefungwa mikono kuongea chochote kuhusiana na taarifa hiyo kwa maelezo kuwa itakuwa imeingia katika kumbukumbu za mahakama.

Na Taus Ally, Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527