LOWASSA : MKAPA AMEGUSIA AJENDA YANGU TANGU CCM....CHADEMA


Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa amemueleza Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa kwamba kauli yake aliyoitoa juzi akitaka kuwepo kwa mjadala wa kitaifa kujadili hali ya elimu nchini ilikuwa ajenda yake tangu alipokuwa CCM.


Lowassa ametoa kauli hiyo leo Machi 19, 2018 katika taarifa yake kwa vyombo vya habari iliyotolewa na msemaji wake, Aboubakar Liongo.


Katika taarifa hiyo, Lowassa ambaye alijiunga Chadema mwaka 2015 baada ya jina lake kukatwa katika mchakato wa kura za maoni ndani ya CCM kusaka mgombea wake wa urais katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, 2015, amesema suala la elimu pia lipo katika ilani ya uchaguzi ya Chadema.


Juzi jioni katika hafla ya kumuaga Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Profesa Idris Kikula, Mkapa amesema kuna janga katika elimu nchini na kushauri kuitishwa kwa mdahalo wa wazi utakaoshirikisha makundi yote ya jamii kwa ajili ya kujadili suala hilo.


Katika taarifa yake hiyo, Lowassa amesema amesoma na kusikia taarifa ya Mkapa akitaka kuwepo kwa mdahalo wa kitaifa kuhusu kushuka kwa elimu nchini.


“Nimefurahi kuwa Mkapa ameliibua suala hili kwani hiyo ilikuwa ni ajenda yangu ya kwanza tangu nikiwa ndani ya CCM na nje ya CCM. Pia Ilani ya uchaguzi ya Chadema, elimu ndio ilikuwa ajenda kuu na tulisema tutaita mjadala wa kitaifa kuhusu elimu na kuangalia wapi tumekwama na nini kifanyike,” amesema Lowassa.


Lowassa amedai ajenda hiyo sio ya CCM na hawataweza kuisimamia kwa sababu wanataka kuendelea kutawala,ila hawataki Taifa lililoelimika vizuri na linaloweza kuhoji.

Na Bakari Kiango, Mwananchi 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527