KADINALI PENGO AUKANA WARAKA WA PASAKA WA MAASKOFU WA KANISA KATOLIKI

Mwadhama Kadinali Polycap Pengo amesema hakuwa anajua kama kuna waraka utatolewa kuhusu kwaresma na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania huku akisema waraka huo una mazuri mengi japo umechanganya dini na siasa.

Kadinali Pengo ameyasema hayo wakati akiadhimisha ibada ya Jumapili ya matawi huko Bagamoyo katika tamasha la vijana.

"Katika wiki chache zilizopita watu wamekuja kwangu wakaniuliza unaionaje ile barua ya Maaskofu kuhusu Kwaresma mwaka huu? Ninazungumzia hilo na wala mtu asiende aka-quote kitu kingine ndio maana nataka kusema wazi kabisa:-

"Barua ile ijapokuwa hata jina langu mnaliona limeandikwa pale kwamba na mimi ni mmoja wa waandishi au watamkaji...mimi nimeipokea, baadhi yenu mmeshaipokea.

" Kwahiyo sioni namna gani mimi naweza kuwa mwandishi au mhubiri kwenu wa ile barua ambayo imetungwa labda na maaskofu...naamini na baadhi ya maaskofu lakini mimi mwenyewe hata nilikuwa sijaiona, hata nilikuwa sijaambiwa kuna kitu cha namna hiyo kinakuja.

"Tuelewane vizuri, ninaposema hivi sitaki kusema ile barua ni mbaya. Moja tu ni kwamba barua nzima imechanganya vitu viwili; Mwalimu angekuwepo angepiga kelele Maaskofu msichanganye Dini na Siasa. 

"Angepiga kelele sana kuhusu waraka huu katika nyakati zake. Na hilo nawambia sina hofu, muende mkamwambie mtu yeyote nimesema hivi. Ndio wala msione aibu, najua labda hata wengine mmekunja nyuso, kunjeni tu lakini huo ndio msimamo wangu.

"Zipo sehemu katika waraka huo zinazochanganya Dini na Siasa na si kazi ya maaskofu ni kazi yenu wanasiasa mkiwa ni wa CHADEMA, mkiwa ni wa CCM lakini haiwezi kuwa kazi yangu mimi. 

"Siwezi kwanza nikaanza kuchambua na ku-criticize Serikali katika mambo yaliyo yake; sikupewa mamlaka hayo. Na kwanini niwe padri mpaka nikubali kuwa Askofu na huku kumbe wito wangu ni siasa? 

"Itakuwa namsaliti hata yule aliyenipa wito huu. Tuchambue yale yanayohusu imani yetu katika ule waraka. Yale ambayo moja kwa moja yanahusu imani yetu Katoliki na tuyashike tuyazingatie kwa dhati kabisa.

"Lakini yale ya kuanza kusema Serikali ya awamu ya 5 inagandamiza uhuru inafanya nini...wewe Askofu uhuru wa kisiasa umeujua wapi? Umeujuaje? Na mambo ya ndani ya kisiasa huyajui na bado uje kutamka...nadhani tumeelewana.

"Yapo yaliyo mema mazuri kabisa katika waraka ule ingawaje sikujuia kama yameandikwa lakini siwezi kukataa yaliyo mema kwa sababu sikujua. 

"Yanaendelea kuwa mema mpaka kesho na keshokutwa. Lakini yale ambayo yanachanganya Dini na Siasa hayo siwezi kuyakubali. 

"Nyerere alifanya indoctrination kubwa mno kwa watu wa umri wetu. Mtu huwezi ukathubutu na ukalala salama usiku. Watu wa umri wangu ukichanganya dini na siasa utaota vitu vya ajabu utakosa usingizi(vicheko)

"Sasa ninyi vijana ninalotaka ni hili kwamba na ninyi mkichanganya dini na siasa muote vitu vibaya kama hivyo..muote vitu vibaya kabisa hata muone mnachungulia kaburi katika ndoto. 

"Sisi sio wanasiasa tunahitaji wanasisia mtuendelee wale tunaokuwa wito huo. Wale tunaotaka kuwa mama wakuu, mababa padri, maaskofu. Fuateni wito kulingana na misimamo yake ya kiimani."

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527