TUME YA UCHAGUZI (NEC) YAJIBU TUHUMA ZA MBOWE


 
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Tume ya Taifa ya Uchaguzi imesikia malalamiko yaliyotolewa na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambayo aliyawasilisha jana kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

Malalamiko yaliyotolewa na Mhe. Mbowe yametusikitisha kwa sababu mbali na kumjibu kwa barua, Mkurugenzi wa Uchaguzi Kailima Ramadhani aliongea na Mhe. Mbowe kwa njia ya simu. Madai kwamba tume haikuwajibu malalamiko yao sio kweli. Ni upotoshaji wa hali ya juu ambao haupaswi kufanywa na kiongozi kama yeye. 

Tume ya taifa ya uchaguzi haijibu malalamiko kwa matakwa ya mtu anavyotaka kujibiwa, bali inajibu hoja kwa mujibu matakwa ya katiba, sheria, kanuni na maadili ya uchaguzi na maelekezo yote ambayo yapo kwa mujibu wa sheria. Kama majibu ya tume hayakuwafurahisha CHADEMA, tume inasisitiza kuwa walijibiwa kwa matakwa ya sheria na katiba na sio matakwa ya mkurugenzi wa uchaguzi, Tume, Chadema au chama chochote cha siasa. 

Kanuni, sheria, maelekezo na maadili ya uchaguzi yameweka utararatibu wa kushughulikia malalamiko na changamoto zinazojitokeza wakati wa uchaguzi. Utaratibu uko wazi kwa changamoto zinazotokea wakati wa uteuzi, wakati wa kampeni ambako kuna kamati za maadili na jinsi ya kukata rufaa.

Kwa masikitiko CHADEMA walitekeleza hatua moja tu katika vipengele hivyo wakati wa uchaguzi, kipengele walichotekeleza ni pale baadhi ya wagombea wao walipoenguliwa kugombea, walifuata utaratibu kwa kuwasilisha rufaa tume ya uchaguzi na Tume ilipitia na ikawarudisha wagombea wao kwenda kugombea.

CHADEMA walitaka wakati wa kampeni, Tume ifanye maamuzi kinyume cha maadili waliyoyasaini. Wakati wa kampeni kuna kamati za maadili ngazi ya jimbo ambayo mwenyekiti ni msimamizi wa uchaguzi na wajumbe ni kutoka vyama vyote vilivyosimamaisha wagombea na ndio wanaofanya uamuzi. Chadema waliwasilisha malalamiko kwa Tume badala ya kuwasilsiha malalamiko kwenye kamati hizo za maadili zinazosimamia malalamiko yote.

Sio sahihi kusema Tume hatukujibu malalamiko yao. Mfano tarehe 15 Chadema waliwasilsiha barua mbili Tume ya Uchaguzi, waliwasilisha barua moja asubuhi na saa 1.30 jioni waliwasilisha barua nyingine, jumla barua hizo zikiwa na hoja tano na Tume ikawaandikia barua zenye ufafanuzi wa hoja hizo. 

Hoja ya kwanza, CHADEMA walitaka kuapishwa mawakala wao mbadala asilimia 15. Tuliwajibu kwamba hakuna kifungu cha sheria kinachokipa fursa chama chochote cha siasa kuapishiwa mawakala mbadala asilimia 15. Kifungu 57 (3) kinafafanua vizuri namna ya mawakala wanavyotakiwa kuwepo na kuapishwa 

Lakini pia hata kama kifungu hicho kingekuwa kinatoa fursa hiyo, Chadema walileta malalamiko yao tarehe 15 Februari 2018 wakati uteuzi wa mawakala ulikuwa tarehe 10 Februari 2018, hivyo hakukuwa na muda wa kuwaapisha mawakala wengine kwa mujibu wa sheria kwa kuwa hawakuwemo kwenye orodha.
Hoja nyingine ya CHADEMA ni msimamizi wa uchaguzi wa Jimbo la Kinondoni alikataa kuwapa mawakala barua na fomu za viapo. Tulifanya hesabu tukaona kwamba msimamizi alitakiwa kusaini barua 22,000 na fomu za viapo 14,000. Tukasema kwamba kutakuwa na utaratibu wa mawakala kupewa fomu na viapo vyao kupitia kwa wawakilishi wao na walipewa kwa njia hiyo. Hili tuliwajibu hivyo katika barua yetu.

Hoja nyingine mawakala wa CHADEMA waliambiwa kwenda na vitambulisho kwenye vituo vya kupigia kura. Katika hoja hii tuliwajibu kwamba wakala chama cha siasa ni mpiga kura kama walivyo wapiga kura wengine. Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kuzingatia sheria ya uchaguzi kifungu namba 61 na namba 62 cha sheria za Serikali za mitaa, Tume ilitoa ridhaa kwa wapiga kura kutumia vitambulisho mbadala ili nao waweze kupiga kura ndio maana wakaelekezwa kwenda navyo.

Hoja nyingine ni kwamba msimamizi wa uchaguzi jimbo la Kinondoni, hajatoa maelekzo ni wapi pa kuhesabia kura. Tukawajibu kwamba Tume ina barua kutoka kwa msimamizi wa uchaguzi akiwajulisha vyama vya siasa kwamba sehemu ya kujumlishia kura itakuwa ni sehemu ya Biafra. Kanuni inasema wangejulishwa eneo hilo la kujumlishia baada ya kura kupokelewa, lakini msimamizi wa uchaguzi alijiongeza akawajulisha mapema eneo la kujumlishia kura.

Hoja nyingine ni wasimamizi wa vituo hawakuteuliwa kwa utaratibu. Majibu ya hoja hii ni kwamba sheria ya uchaguzi imeweka utaratiibu wa namna wasimamizi hao wanavyopatikana. Lakini kanuni za uchaguzi wa Rais namba 15 na kanuni 11 za Serikali za Mitaa zinaeleza namna msimamizi wa kituo anavyopatikana.

Kanuni hiyo inasisitiza kuwa msimamizi wa uchaguzi atatoa tangazo, Kwa jimbo la Kinondoni msimizi alitoa tangazo, watu waliomba, walifanya usahili na kabla ya uteuzi mkurugenzi wa uchaguzi alitoa matangazo ya majina katika mbao zote za kata 10 za jimbo la Kinondoni. 

Msimamizi wa uchaguzi aliwaandikia barua vyama vyote kama vina pingamizi vijitokeze. Kama kulikuwa na tatizo vyama vilikuwa na fursa ya kuweka pingamizi, lakini hawakufanya hivyo na Tume tuliwajibu hivyo. Unaposema tume haikuwajibu sio kweli, labda CHADEMA waseme tuliwajibu nje ya matakwa yao waliyotaka na sio kwa mujibu wa sheria.

Hoja nyingine ni kwamba kuna wizi wa kura. Katika kituo cha kupigia kura kuna msimamizi wa kituo, msimamizi msaidizi na wakala wa chama cha siasa na kuna waandishi wa habari. Utaratibu ulikuwa wazi. Pia kuna utaratibu wa kisheria wa kuwasilisha malalamiko kama mtu haridhiki kabla wakati na baada ya kupiga kura, wakati wa kuhesabu na baada ya kuhesabu kura.

Mtu au chama kisipofuata uratibu huo, lazima utalalamika tu na utaona tume ni korofi. Hii ni kwa sababu mtu akija Tume kulalamika, ataelekezwa kufuata utaratibu huo. Mgombea akikataa kufuata utaratibu huo hata akija Tume kulalamika,ataelekezwa na Tume atumie wakala wake kujaza fomu zote namba 14 na 16 zinazohusika kisheria kuwasilisha malalamiko.

Tunamsihi Mbowe na chama chake, wasome sheria za uchaguzi na kuzielewa. Tume iko tayari kumpa elimu ya mpiga kura kuzifahamu sheria hizi kwa mapana yake.

Pia tunamwomba Mhe. Mbowe kama hakuridhika na taratibu za uchaguzi, ana fursa ndani ya siku 30 za kuwasilisha malalamiko yake mahakamani ndicho chombo pekee cha kutoa haki. Aende mahakamani kwa kutumia ushahidi ambao mawakala wake walijaza kwenye fomu namba 14 na 16 kwa sababu Tume ya Uchaguzi haina tena fursa ya kupokea malalamiko kisheria baada ya uchaguzi kupita.

Kailima, R.K

MKURUGENZI WA UCHAGUZI

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post