KIONGOZI WA CHADEMA ALIYEUAWA KUZIKWA IJUMAA WIKI HII


Mwili wa aliyekuwa Katibu wa Chadema Kata ya Hananasif jijini Dar es Salaam, Daniel John unatarajiwa kusafirishwa kesho kwenda Iringa kwa maziko. 

John ambaye ni mpigapicha maarufu Hananasif aliuawa na watu wasiojulikana na mwili wake uliokotwa jana kwenye fukwe za Coco.

Akizungumzia maandalizi ya mazishi ya kiongozi huyo, mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko ambaye anasimamia kampeni za Chadema katika kata hiyo amesema marehemu atasafirishwa kesho na kuzikwa Ijumaa wiki hii.

Matiko amesema vikao vya kukusanya fedha kwa ajili ya kusafirisha mwili wa mwanachama wao huyo vinaendelea kufanyika na kesho wanatumaini kusafirisha kwenda Mafinga mkoani Iringa.

"Tumewasiliana na familia ya marehemu wametaka ndugu yao akazikwe Iringa. Tunafanya jitihada za kukusanya fedha ili kufanikisha mazishi ya kiongozi wetu," amesema.

Mbunge huyo amelitaka Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi na kuchukua hatua dhidi ya watu waliohusika kukatisha maisha ya kijana huyo 

Matiko amebainisha kuwa ana uhakika asilimia 100 kwamba hayo ni mauaji ya kisiasa kwa sababu marehemu alitishiwa maisha na watu ambao wanafahamika.

Akizungumzia mazingira ya kifo cha mumewe, mjane wake, Paulina Vitalis amesema kuna watu walikwenda nyumbani kwake Jumapili, Februari 11 kumuulizia mumewe akawaambia hayupo.

Amesema baada ya kuwajibu hivyo waliuliza tena kuwa muda anaorudi nyumbani, akawajibu saa nne usiku 

Amesema siku hiyo mumewe hakurudi nyumbani mpaka jana Jumanne ambapo alipata taarifa kwamba mumewe alikuwa ameuawa na mwili kuokotwa kandokando ya fukwe za Coco.

"Hakuna siku mume wangu aliwahi kuniambia kwamba anatishiwa maisha, lakini Jumatatu watu ndio waliniambia kwamba kuna watu walikuwa wanamtafuta sana," amesema mwanamke huyo ambaye alizaa mtoto mmoja na mwanasiasa huyo.

Akizungumza kwenye msiba huo nyumbani kwa marehemu Mtaa wa Kawawa , Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema kuuawa kwa John ni njama za washindani wao kwenye uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kinondoni ili kuwapunguza nguvu. 

Amewataka viongozi na wanachama wa Chadema kutorudi nyuma, bali waendelee na kampeni kama kawaida wakati watu wachache wakiratibu shughuli za mazishi ya kiongozi wao.

"Wenzetu wameamua kuua ili tu washinde uchaguzi huu, tusikubali kuvurugwa na msiba tukasahau uchaguzi. Tukifanya hivyo, lengo lao litakuwa limetimia," amesema Mbowe.

Amewataka wanachama wawe watulivu wakati shughuli za kupumzisha mwili wa marehemu zikiendelea na washirikiane na viongozi wanaoratibu mazishi katika kufanikisha suala hilo.

Awali, akizungumza kwenye msiba huo, mbunge wa viti maalumu, Susan Lyimo amesema hali ya kisiasa nchini sasa si nzuri kwa sababu viongozi hawataki kukosolewa.

"Hawataki kuona kiongozi anatoka Chadema ndio maana wanatumia nguvu nyingi kuwadhibiti. Mtakumbuka Alphonce Mawazo aliuawa, Tundu Lissu naye alipigwa risasi na kunusurika kuuawa," amesema Lyimo.

Na Peter Elias, Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527