UAMUZI WA KESI YA WANAWAKE WALIOVALISHANA PETE YA UCHUMBA KUJULIKANA KESHO

Hatima ya dhamana ya washtakiwa wanne wanaokabiliwa na kesi ya kujihusisha na vitendo vinavyoashiria mapenzi ya jinsia moja na makosa ya mtandao itajulikana Ijumaa Desemba 15,2017 Mahakama ya Hakimu Mkazi Mwanza itakapotoa uamuzi.


Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi, Wilbert Chuma anayesikiliza shauri hilo aliliahirisha baada ya kusikiliza hoja kuhusu hati ya kiapo iliyowasilishwa na Jamhuri kuzuia dhamana.


Washtakiwa katika shauri hilo namba 548/2017 ni Milembe Suleiman na Janeth Shonza, mwanafunzi wa sheria katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine wanaodaiwa kuvishana pete ya uchumba licha ya wote kuwa wanawake.


Wengine ni Aneth Mkuki anayedaiwa kufanikisha sherehe ya wawili hao kuvishana pete na Richard Fabian, anayeshtakiwa kwa kosa la mtandao kwa kusambaza video za tukio hilo kwenye mitandao ya kijamii.


Akiwasilisha hati iliyosainiwa na Mkuu wa Upelelezi Mkoa (RCO) wa Mwanza, John Ndibalema, Wakili wa Serikali Emmanuel Luvinga aliiomba Mahakama kuzuia dhamana ya washtakiwa kwa sababu wakiwa nje wanaweza kuingilia upelelezi wa kesi ambao haujakamilika.


Luvinga alidai jana kitendo walichokifanya washtakiwa ni kinyume cha maadili, jambo linaloweza kusababisha wadhuriwe na jamii iliyoangalia video ya wao kuvishana pete kupitia mitandao ya kijamii.


“Ni rai ya upande wa Jamhuri kuwa washtakiwa waendelee kushikiliwa mahabusu kwa usalama wao,” alisema wakili Luvinga.


Mawakili wa utetezi Mashaka Tuguta, Ogastini Kulwa na Jebra Kambole waliwasilisha hati kinzani kupinga hoja hizo wakisema licha ya dhamana kuwa haki ya washtakiwa na shauri linalowakabili kuwa na dhamana, msingi wa hoja za zuio ni hisia.


Upande wa utetezi ulisema jukumu la upelelezi na ulinzi wa washtakiwa ni la upande wa Jamhuri, hivyo hoja hiyo isitumike kuwanyima haki washtakiwa.


“Hoja zilizomo kwenye hati ya kiapo kuzuia dhamana ya washtakiwa zimejengwa kihisia kwa sababu haionyeshi namna gani washtakiwa watadhurika wala idadi ya walioona video wanaodaiwa kuchukizwa,” alisema wakili Tuguta.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post