RAIS MAGUFULI AANZA ZIARA YA SIKU TATU UGANDA

 Rais John Magufuli ameanza ziara rasmi ya kiserikali ya siku tatu nchini Uganda kwa mwaliko wa Rais Yoweri Museveni.

Dk Magufuli aliyeongozana na mkewe Janeth amewasili Mtukula mpakani mwa Tanzania na Uganda ambako amepokewa na mwenyeji wake Rais Museveni aliyeambatana na mkewe Janeth.

Katika mapokezi hayo leo Alhamisi Novemba 9,2017, Rais Magufuli amepigiwa mizinga 21 na amekagua gwaride lililoandaliwa kwa heshima yake.

Wakiwa mpakani, viongozi hao wawili watafungua kituo cha pamoja cha huduma za mpakani (One Stop Border Post - OSBP) kilichojengwa ili kurahisisha utaratibu wa forodha, uhamiaji na kuharakisha biashara kati ya nchini hizi mbili.

Taarifa ya Ikulu imesema baadaye leo, marais hao wataweka jiwe la msingi katika mradi wa bomba la mafuta ghafi linaloanzia Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga nchini Tanzania.

Shughuli hiyo itafanyika katika Kijiji cha Luzinga, kilichopo mkoani Rakai nchini Uganda.

Baada ya ufunguzi, viongozi hao watazungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara utakaofanyika wilayani Kyotera nchini Uganda.

Rais Magufuli jioni ya leo atahudhuria dhifa ya kitaifa iliyoandaliwa kwa heshima yake na Rais Museveni katika mji wa Masaka.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post