Picha : DC SHINYANGA AIBUKIA KWENYE SHAMBA DARASA LA PAMBA KUANZA RASMI MSIMU WA KILIMO CHA PAMBA

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro ameshiriki katika kilimo cha pamba katika shamba darasa lililoanzishwa katika kijiji cha Solwa kata ya Solwa katika halmashauri ya wilaya ya Shinyanga.

Shamba darasa hilo litatumika kama darasa la kilimo cha pamba kwa njia za kitaalamu kwa wakulima wa pamba katika wilaya hiyo katika msimu hu wa kilimo cha pamba ili waweze kuvuna mazao mengi na kujiongezea kipato pia kuondokana na uhaba wa chakula.

Matiro ambaye alikuwa ameambatana na wataalamu pamoja na viongozi wa kata ya Solwa ,mkurugenzi wa halmashauri hiyo Bakari Mohamed 
Novemba 24,2017,amepanda zao la pamba kwenye shamba darasa la kata hiyo. 


Akizungumza wakati wa kupanda pamba katika shamba hilo Matiro aliwataka wakulima wa halmashauri hiyo kuiga mfano wa kilimo cha kitaalamu kinachofanywa kwenye mashamba darasa kwa kutumia kamba.

“Lengo la mimi kuingia shambani na kuanza kupanda zao la pamba pamoja na viongozi wa kata hii ni kuhamasisha wakulima kulima kitaalamu ili waweze kupata mavuno mengi kwani wakizembea hakuna wa kuwaletea chakula na serikali haina shamba hivyo wajitahidi kufuata maelekezo ya wataalamu ili kujiinua kiuchumi kupitia zao hili la biashara”,alisema Matiro. 


Hata hivyo alisema katika msimu huu wa kilimo cha pamba serikali imejitahidi kuleta mbegu bora za aina zote kwa wakulima.

Matiro alisisitiza kila kata iwe na shamba darasa litumike kama mfano kwa wakulima na kila shule kupanda zao la mtama kwa wingi.

Mkuu huyo wa wilaya aliwasisitiza wakulima pia walime na mazao mengine kama zao la mtama linalostahimili ukame ili kukabiliana na njaa.

Akiongea kwa niaba ya wakulima diwani wa kata hiyo Awadhi Aboud alisema shamba darasa hilo hilo lina ukubwa wa zaidi ya ekari tano wakulima tayari wamefahamu jinsi ya kulima kilimo cha kitaalamu.

Ofisa kilimo wa halmashauri hiyo Edward Maduhu alisema kilimo wanacholima wakulima kisicho cha kitaalamu kwa zao la pamba wanaweza kuvuna kilo 300 hadi 400 kwa ekari moja lakini wakilima kitaalamu wana uwezo wa kuvuna tani 800 hadi zaidi ya 1000 kwa ekari hiyo.

“Kitaalamu ekari moja inatakiwa kuwepo kwa miche 22,222 lakini wakulima wa zao la pamba wanapokuwa hawajapanda kitaalamu ni vigumu kuifikia miche hiyo, siku zote inakuwa pungufu hata mavuno huwa ni kidogo sababu huacha nafasi kubwa na kutofikia idadi inayohitajika ya miche”,alisema Maduhu.

Msimu mpya wa kilimo cha pamba mwaka 2017/2018 katika Kanda ya Magharibi inayojumuisha mikoa ya Mwanza, Simiyu, Shinyanga, Geita, Tabora, Mara, Kagera, Singida, Kigoma na Katavi, umezinduliwa rasmi wiki hii kwa upandaji pamba utakaoendelea hadi mwishoni mwa mwezi ujao.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Pamba Tanzania (TCB), Marco Mtunga,katika msimu wa kilimo wa 2017/2018 jumla ya tani 25,000 za mbegu zimetengwa, zikijumuisha tani 11,548 za mbegu mpya ya UKM08 na tani 13,452 za mbegu ya UK91.

Usambazaji wa mbegu ulianza Septemba 15, mwaka huu na ukitarajiwa kukamilika Novemba 30, mwaka huu, ambapo jumla ya ekari 1,300,000 zinatarajiwa kupandwa katika msimu wa kilimo kwa mwaka huu katika kanda hiyo.


ANGALIA HAPA CHINI PICHA ZA SHAMBA DARASA KATA YA SOLWA
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akiwa amebeba mfuko wa mbegu za pamba,kushoto ni diwani wa kata ya Solwa,Awadhi Aboud

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akiwa ameshikilia mfuko wa mbegu za pamba
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akipanda pamba katika shamba darasa
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro na diwani wa kata ya Solwa Awadhi Aboud wakiwa shambani
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akipanda pamba
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine akiwa katika shamba la pamba


Kulia ni Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Bakari Kasinyo Mohamed akiwa katika shamba darasa

Kushoto ni Afisa tawala wilaya ya Shinyanga Charles Maugira akishiriki zoezi la kupanda pamba

Zoezi la kupanda pamba linaendelea


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post