ZITTO KABWE AACHIWA KWA DHAMANA KESI YA MAKOSA YA MTANDAO NA SHERIA YA TAKWIMU

Mbunge wa Kigoma Mjini na kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe ameachiwa huru kwa dhamana na kutakiwa kuripoti siku ya Jumanne saa tatu asubuhi kwa Mkurugenzi wa upelelezi wa Makosa ya jinai (DCI) jijini Dar es Salaam.


Mwanasheria wa Zitto Kabwe amesema kuwa mpaka sasa mteja wake anatuhumiwa kwa makosa mawili tofauti likiwepo kuchapisha taarifa kinyume cha sheria ya mitandao lakini kosa jingine ni kutoa takwimu za uongo kinyume na kifungu cha 37 (5) cha sheria ya takwimu ya mwaka 2015 hivyo mwanasheria anasema Zitto Kabwe amehojiwa na kutoa maelezo yake hivyo wanasubiri kujua kama watakwenda mahakamani.


Kwa upande wake Zitto Kabwe amefunguka na kusema kwa sasa wanasubiri kuona wanapelekwa mahakamani ili waweze kujadiliana huko na kusema kama wao kuna makosa ambayo wanayaona kwake sehemu pekee ambayo wanaweza kwenda kufafanua vizuri ni mahakamani na kudai kuwa kama asingekamatwa angeshangaa kwa kuwa tayari Rais alikuwa ameshatoa agizo.

"Tunasubiri ni lini watatupeleka mahakamani kwa ajili ya kutetea masuala ambayo tumezungumza lakini ya ziada ni kama ambavyo Mwanasheria amezungumza kwa hapa ni makosa mawili ya Sheria ya Takwimu na Sheria ya makosa ya mitandao, wananchama waendelee kuwa watulivu tu kwa sababu kila mtu alitarajia kuwa tutakamatwa kwa kuwa Rais alisema kuwa nikamatwe hivyo tusingekamatwa ningeshangaa, la ziada ni kwamba tusubiri mahakamani itakuaje" alisisitiza Zitto Kabwe


Mbali na hilo kiongozi huyo wa ACT Wazalendo amewataka wanachama pamoja na viongozi wa chama hicho kuendelea na harakati za uchaguzi mdogo wa udiwani na kusema endapo wakishinda katika uchaguzi huo ni kitu ambacho kitakuwa faraja kwao.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527