WENYE VYETI FEKI WAENDELEA KUKABWA KOO..SASA SERIKALI KUWAFUNGULIA KANZI DATA WASIAJILIWE


SEKRETARIETI ya Ajira katika Utumishi wa Umma imebainisha kuwa bado kuna baadhi ya waombaji wa kazi za utumishi wa umma wanaoendelea kughushi sifa za kielimu, taaluma na taarifa binafsi pamoja na hatua kali zinazoendelea kuchukuliwa na serikali.

Kutokana na taarifa hiyo, serikali imeagiza sekretarieti hiyo kufungua kanzi data ya kutengeneza orodha ya watu wote wanaoomba ajira kupitia chombo hicho watakaobainika kufanya udanganyifu kupitia vyeti vyao ili wawekewe zuio la ajira za utumishi wa umma serikalini.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki aliagiza sekretarieti hiyo kuwachukulia hatua waombaji wote watakaobainika kuwasilisha taarifa za taaluma zenye udanganyifu ikiwa ni pamoja na kuanzisha kanzidata yenye orodha yao ili wawekewe zuio la ajira serikalini.

“Naomba utaratibu uwekwe wa kuwasajili watu hawa wadanganyifu kupitia kanzidata na kuwa ‘black listed’ (kuwafungia), orodha hii ipelekwe kwenye ofisi zote na taasisi zote za serikali ili wasipate ajira kwa njia yoyote, lakini pia washitakiwe kwa kuthubutu kuja kwenye chombo kizito kama hiki na kudanganya,” alifafanua Kairuki.

Aidha, imebainika kuwa baada ya ajira kufunguliwa katika mwaka wa 2017/18, sekretarieti hiyo imepokea vibali vya ajira 292 vyenye jumla ya idadi ya nafasi 2,611 na hadi kufikia Septemba mwaka huu, waombaji 185 wameshapangiwa vituo vya kazi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa bodi mpya na Mkataba wa Huduma kwa Mteja ya Sekretarieti hiyo ya Ajira katika Utumishi wa Umma, Katibu wa Sekretarieti hiyo, Xavier Daudi alisema kughushi vyeti bado ni changamoto wanayoendelea kukumbana nayo.

Daudi alisema pamoja na chombo hicho kimeanza kuchukua hatua ikiwa ni pamoja na kufuatilia vyeti hivyo vya kughushi vinapotolewa na kwamba imebaini taasisi zinazotambulika zinazotoa vyeti hivyo.

“Hili tumeliona hasa kwenye nafasi za udereva, kuna vyuo vya udereva vya mitaani tena vilivyosajiliwa na Vyuo Ufundi vya Veta, tulipofuatilia na kuvihoji baadhi yake kuhusu vyeti hivi vya kughushi vimekiri kuwa vyeti hivyo ni vyao.

Hili ni tatizo kwa kweli,” alisema Daudi. Katibu huyo alisema baada ya ajira kufunguliwa katika mwaka wa 2017/18, sekretarieti hiyo imepokea vibali vya ajira 292 vyenye jumla ya idadi ya nafasi 2,611 na hadi kufikia Septemba mwaka huu, waombaji 185 wameshapangiwa vituo vya kazi.

“Katika juma lijalo tunatarajia kuwapangia vituo vya kazi zaidi ya wasailiwa 400 ambapo pia tuna vibali vingi ambavyo vipo kwenye hatua mbalimbali,” alieleza. “Naomba niweke wazi kuwa chombo hiki hakikuanzishwa kwa bahati mbaya, kilianzishwa kwa ajili ya kutatua changamoto za ajira nchini kutokana na matatizo kadhaa yaliyokuwepo huko nyuma kama vile kuajiri bila kuzingatia sifa, ukabila, udini, undugu na urafiki, na gharama kubwa za matangazo ya ajira,” alieleza.

Pamoja na hayo, waziri huyo aliagiza sekretarieti hiyo, kuhakikisha inafanya mchakato wa ajira kwa kuzingatia taratibu, kanuni na sheria za ajira zilizopo na kupata watumishi wa umma wenye sifa stahiki, hivyo kuisaidia Serikali kutekeleza mipango yake ya kiuchumi na kimaendeleo.

“…Naomba muendelee kuwa wabunifu na kutumia mbinu za kisasa katika kutekeleza majukumu yenu ili rasilimali watu mnayoiandaa ikidhi matarajio ya wadau wenu pamoja na taifa kwa jumla,” alisema Waziri Kairuki. Alisema chombo hicho kikitoa wasailiwa bora wanaokidhi mahitaji ya waajiri, watasaidia taifa kufikia malengo iliyojiwekea ikiwemo kuijenga Tanzania.

IMEANDIKWA NA HALIMA MLACHA - habarileo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post