DAKTARI ALIYEACHA WAGONJWA NA KWENDA KULEWA POMBE APATWA BALAA


WAZIRI wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto, Ummy Mwalimu amemwelekeza Naibu Katibu Mkuu Tamisemi, Dk Zainab Chaula kumchukulia hatua daktari wa Hospitali ya Wilaya ya Maswa, Laurent Biyengo aliyedaiwa kushindwa kuingia kazini na kwenda kunywa pombe na kusababisha wagonjwa kutopatiwa huduma.

Aidha, Polisi wilayani humo imethibitisha kumkamata na kumseka ndani daktari huyo kwa maagizo ya Mkuu wa wilaya hiyo, Dk Seif Shekalaghe. Hatua imefikiwa baada ya baadhi ya wagonjwa waliofika katika hospitali hiyo Septemba 27, mwaka huu saa 1:00 hadi saa 3:30 usiku kukosa huduma kutokana na kutokuwepo kwa daktari huyo wa zamu na kusababisha ujauzito aliokuwa nao Salome John kutoka na kuharibika wakati akimsubiri daktari huyo aliyekwenda kulewa.

Waziri Ummy ametoa maelekezo hayo kwa njia ya simu baada ya kupata taarifa hizo kwa njia ya ujumbe mfupi wa maandishi (SMS) kutoka gazeti hili(Habarileo) juu ya wagonjwa waliofika kupata huduma katika hospitali hiyo na kumkosa daktari wa zamu.

Wagonjwa waliopatwa na madhira hayo wakizungumza na waandishi wa habari katika Hospitali ya Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu walisema walifika asubuhi katika hospitali hiyo kwa ajili ya kupata matibabu, lakini cha kushangaza daktari wa zamu hakuwepo.

Walidai licha ya wauguzi kuwepo, lakini walishindwa kuwahudumia hasa mjamzito, Salome John aliyekuwa akilia kutokana na maumivu aliyokuwa akiyapata kwa maelekezo kuwa taratibu haziruhusu ni hadi hapo watakapoandikiwa cheti na daktari hali iliyosababisha mgonjwa huyo ujauzito wake kutoka.

“Nilimleta mwanangu akiwa ana mimba mara baada ya kunieleza ya kuwa anahisi maumivu makali tumbo tulifika hospitali majira ya saa 1:30 usiku, lakini daktari hatukumkuta licha ya kuandikiwa cheti lakini tulibaki kumsubiri daktari lakini hakuonekana ilipofika saa 3:20 usiku maumivu yalimzidi binti yangu na wauguzi walikataa kutuhudumia hadi tumwone daktari na hatimaye mimba yake ikatoka,” alidai Suzana Kalumbilo ambaye ni mama mzazi wa Salome.

Kwa mujibu wao, baada ya kuona hali inazidi kuwa mbaya kwa wagonjwa waliokuwepo walichukua jukumu la kumpigia simu Mkuu wa wilaya, Dk Shekalaghe ambaye naye alichukua jukumu la kumpigia simu Mganga Mkuu wa Wilaya, Dk Jonathan Budenu.

Walisema Dk Budenu aliyefika muda mfupi baada ya kupigiwa simu na DC wake, alifanya jitihada za kupata daktari mwingine ambaye alifika na kuanza kutoa huduma kwa wagonjwa waliokuwepo. 

Inaelezwa kwamba ilipofika saa 3:40 usiku ndipo Bihengo alipofika akiwa amelewa huku hajitambui na kuingia katika chumba cha daktari, lakini Mganga Mkuu wa Wilaya, Dk Budemu alimtoa na kumtaka asitoe huduma yoyote kutokana na hali aliyokuwa nayo.

IMEANDIKWA NA SHUSHU JOEL-HABARILEO MASWA

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post