WANAJESHI WAWILI WA TANZANIA WAUAWA KONGO


Askari wawili wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Tanzania, wameuawa kwenye mashambulizi makali yanayoendelea nchini Kongo.


Tukio hilo limetokea katika eneo la Beni ambako Askari wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani wanapigana na kikundi cha waasi cha Uganda (ADF), kilichoanza vurugu na ukiukaji wa haki za binadamu kwa kuua raia.


Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amethibitisha kuuawa kwa wanajeshi hao kutoka Tanzania, huku akitoa tarifa kuwa askari wengine 18 kutoka nchi tofauti wamejeruhiwa.


Pamoja na hayo Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amehimiza mamlaka za Kongo kuchunguza haraka tukio hilo na kuwachukulia hatua wahusika.


Hivi karibuni nchini Kongo kumekuwa na machafuko baada ya vikundi vya uasi kuanza tena vurugu na mauaji baada ya miaka kadhaa kupita kukiwa shwari, huku serikali ya nchi hiyo na Umoja wa Mataifa wakiishtaki ADF kwa ukiukaji wa hai za binadamu na mauaji ya watu zaidi ya 700 katika eneo la Beni, tangu Oktoba 2014.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post