MAJAJI WAPEWA ANGALIZO KUHUSU MATUMIZI YA MITANDAO YA KIJAMII

Jaji Mkuu Profesa Ibrahim Hamis Juma, ametoa angalizo kwa Majaji wafawidhi kuwa makini na matumizi ya mitandao ya kijamii katika mahusiano pamoja na kutoa michango kwenye mitandao hiyo juu ya jumbe zisizofaa.


Jaji Mkuu ametoa angalizo hilo wakati akifunga mkutano wa Majaji wafawidhi wa kanda nchini, uliofanyika Jijini Arusha


"Katika suala la matumizi ya mitandao, kuweni makini. Msi- like picha ambazo hazina maadili au kuchangia kwa kutoa maoni katika mitandao ya kijamii," alisema.


Aidha, amewataka kuwa makini na ndugu au jamaa wanaowatembelea, akisema baadhi yao wanatuhumiwa na makosa mbalimbali ya kijinai.


Aliwataka majaji hao kujenga tabia ya kupenda kujisomea na kuelewa mabadiliko yanayofanywa na Bunge kwa kurekebisha sheria ili kuweza kugundua makosa mbalimbali yanayofanywa na Mahakama za chini na wafundishane namna ya kuboresha hukumu zinazotolewa ili kupunguza mrundikano wa mashauri.


"Ni vizuri kuelewa mabadiliko yanayofanywa na Bunge wakati wa kurekebisha sheria, kazi na hatua zinazotakiwa kuchukuliwa katika kufungua mashauri," alisema.


Kuhusu migongano kati yao na vyombo vingine vya serikali, aliwataka kutambua mipaka ya vyombo hivyo na wao watambue mipaka yao huku akisisitiza kwamba kila chombo kikitambua mipaka yake wataheshimiana na hakutakuwa na mgongano katika utekelezaji wa majukumu yao.


Mkutano huo wa majaji wafawidhi ulikuwa mahususi kutathmini na kuweka mikakati ya kumaliza mrundikano wa mashauri 2,198 yaliyopo Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani, kati yao mengine yamekaa zaidi ya miaka 10.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post