Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto amezungumzia tukio la kupigwa risasi mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, akiwaomba wananchi wenye taarifa kulisaidia jeshi hilo.
Muroto amesema leo Alhamisi kuwa wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo na wameshafika eneo la tukio nyumbani kwa Lissu.
“Tunaomba mwananchi wenye taarifa atusaidie. Jeshi la Polisi tumeanza uchunguzi, tumefika eneo la tukio na tunaendelea,” amesema.
Kamanda Muroto amesema taarifa za awali zinaonyesha kuna gari aina ya Nissan lenye rangi nyeupe lilikuwa likimfuatilia Lissu.
Katika mkutano na waandishi wa habari, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana amewataka wananchi kuwa watulivu wakisubiri taarifa za Jeshi la Polisi na madaktari wanaoendelea na matibabu ya mbunge huyo, ambaye pia ni mwanasheria mkuu wa Chadema.
Akizungumza maendeleo ya matibabu ya mwanasiasa huyo ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma James Charles amesema Lissu yu hai na imara.
Amsema mbunge huyo amepigwa risasi tumboni na kwamba timu ya madaktari inaendelea na matibabu.
“Tumempokea Lissu mchana, kanuni za matibabu haziruhusu mtu mwingine asiye mtumishi kuingia chumba cha matibabu. Tuna uwezo wa kutosha wa kutoa huduma ya dharura,” amsema.
Amsema kwa sasa wanaendelea na huduma na wakikamilisha watatoa taarifa.