HALMASHAURI YA KISHAPU YATENGA BAJETI YA MILIONI 4.7 KUSAIDIA TAULO LAINI 'PEDS' KWA WANAFUNZI WALIOKO KWENYE HEDHIAfisa Maendeleo ya Jamii wa halmashauri ya Kishapu,Joseph Swalala akizungumza katika Tamasha la Jinsia mwaka 2017 katika viwanja vya TGNP Mtandao jijini Dar es salaam-Picha na Kadama Malunde-Malunde1 blog


Halmashauri ya wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga imetenga bajeti ya shilingi milioni 4.7 katika bajeti ya mwaka 2017/2018 kwa ajili ya kununua taulo laini ‘Peds’ kwa ajili ya wanafunzi wa kike katika shule zote za sekondari wilayani humo kujisitiri wanapokuwa kwenye hedhi.

Akizungumza leo Alhamis Septemba 7,2017 kwenye Tamasha la Jinsia la 14 mwaka 2017 lililoandaliwa na TGNP Mtandao linalofanyika jijini Dar es salaam,Afisa Maendeleo ya Jamii wa halmashauri ya Kishapu,Joseph Swalala alisema hatua hiyo itawasaidia wanafunzi wengi kuhudhuria masomo yao shuleni.

Swasala alisema wanafunzi wengi wa kike wanapokuwa katika hedhi hushindwa kuhudhuria masomo yao shuleni kwa wastani wa siku tatu kwa mwezi kwa vile huchukulia kuwa hedhi ni ugonjwa.

“Madiwani katika halmashauri yetu wamekubali kupitisha bajeti ya shilingi milioni 4.7 kupitia Idara ya Maendeleo ya Jamii kwa ajili ya taulo laini kwa wanafunzi wa kike katika shule za sekondari,na tutaanza na wanafunzi 256”,alieleza Swalala.

“Tulibaini kuwa hedhi ni miongoni mwa sababu zinazochangia watoto wa kike kutohudhuria masomo yao hivyo kushindwa kufaulu vizuri kwenye mitihani yao”,aliongeza Swalala.

Alisema wanachofanya hivi sasa ni kuhakikisha katika kila shule kunawepo na vyumba maalumu kwa ajili ya watoto kujistiri lakini kuwa na walimu walezi kwa ajili ya kuwasaidia watoto wa kike wanapokuwa katika hedhi.

Akizindua Tamasha la Jinsia mwaka 2017,Makamu wa Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan alikabidhi tuzo kwa Halmashauri ya Kishapu mkoa wa Shinyanga na Kisarawe mkoa wa Pwani kwa kutenga bajeti inayozingatia masuala ya Kijinsia hususani suala la Hedhi Salama kwa watoto wa kike shuleni.

Na Kadama Malunde- Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post